DPP atoa sababu ya kuondoa kesi ya mauaji dhidi ya mjane wa Tob Cohen

Nyamosi alisema mwaka 2020 waliandika barua mbili kuelekeza timu ya wapelelezi kuangazia maeneo 35 ya uchunguzi

Muhtasari
  • Mwendesha mashtaka pia anasema hata aliagiza kwamba kamanda wa polisi wa kaunti ndogo Gigiri ahojiwe kuhusu maingiliano na uhusiano wake na Sarah
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji
DPP Norrdin Haji Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji
Image: Maktaba

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ametetea uamuzi wake wa kuondoa mashtaka ya mauaji dhidi ya mjane wa Tob Cohen Sarah Wairimu.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Alhamisi, DPP alisema alipitia faili ya mauaji na akapendekeza kesi hiyo isajiliwe kama uchunguzi lakini sio mauaji.

Katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Jacinta Nyamosi, DPP alisema mambo kadhaa yalijitokeza wakati wa uhakiki wa jalada hilo ambayo hayaeleweki na kusababisha kuondolewa kwa shtaka la mauaji.

Lakini pigo kubwa zaidi la kusambaratika kwa kesi hiyo linahusishwa na hati ya kiapo maarufu ya Gachomo ambapo alibatilisha hati za kiapo za awali ambazo zilimhusisha Sarah na mauaji hayo.

“Kuondolewa kwa hati ya kiapo hivi majuzi na John Gachomo kulileta pigo kubwa kwa kesi hiyo. Zaidi ya hayo, iliibua wasiwasi mkubwa kuhusu uadilifu wa mchakato mzima wa uchunguzi,” alisema.

Nyamosi alisema mwaka 2020 waliandika barua mbili kuelekeza timu ya wapelelezi kuangazia maeneo 35 ya uchunguzi ambayo hadi sasa hayajashughulikiwa.

"Taarifa zilizorekodiwa na polisi zinaonyesha kuwa polisi kadhaa waliovalia kiraia walitembelea boma la marehemu Cohen na utambulisho wa maafisa hao bado haujajulikana," Nyamosi alisema.

Mwendesha mashtaka pia anasema hata aliagiza kwamba kamanda wa polisi wa kaunti ndogo Gigiri ahojiwe kuhusu maingiliano na uhusiano wake na Sarah lakini hilo pia halijafanyika.

Anasema pia madai ya kughushi uhawilishaji wa hisa za marehemu Cohen hayajaisha, hivyo kuzua maswali kuhusu ni nani aliyefanya hivyo.

Nyamosi alisema hoja zilizotajwa hapo juu zilisababisha DPP kufanya uamuzi kwamba uchunguzi wa umma lazima ufanyike ili kubaini watu waliohusika na mauaji ya marehemu Cohen.