Mpishi afungwa miaka 40 gerezani kwa kumnajisi bintiye wa miaka 13, kumtunga mimba

Mlalamishi alifanyiwa uchunguzi wa maumivu ya tumbo na kutapika na ikabainika alikuwa mjamzito.

Muhtasari

•Msichana huyo alimweleza mama yake kwamba wakati wa likizo ya shule mshtakiwa alimlazimisha kufanya mapenzi.

•Mshtakiwa alikamatwa akiwa katika Shule ya Wavulana ya Enkii ambako alikuwa akifanya kazi ya upishi mkuu.

Mahakama
Mahakama
Image: MAHAKAMA

Mpishi mwenye umri wa miaka 42 amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 40 jela na mahakama ya sheria ya Loitoktok kwa kufanya mapenzi na binti yake mwenye umri wa miaka 13.

Paulo Orumoi Moonka, ambaye alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Samuel Ndung’u alishtakiwa kwamba mnamo Julai 24, 2021 katika eneo la Kimana, kaunti ndogo ya Loitokitok, alimnajisi mtoto huyo.

Esther Tepenoi Saotet, mamake msichana, alikuwa amesimulia jinsi mnamo Agosti 18, 2021, alipokea simu kutoka kwa matroni wa shule ambapo binti yake alikuwa akisoma na kufahamishwa wamba alikuwa mgonjwa.

Mwanafunzi huyo wa darasa la 7 katika Shule ya Msingi ya Enkii alipelekwa hospitalini na mamake na kufanyiwa uchunguzi wa maumivu ya tumbo na kutapika, jambo lililothibitisha kwamba alikuwa mjamzito.

Baada ya kuhojiwa, msichana huyo alimweleza mama yake kwamba wakati wa likizo ya shule mshtakiwa alimlazimisha kufanya mapenzi na baadaye kutishia kwamba angemuua pamoja na mama yake ikiwa angefichua jambo hilo.

Baada ya ufichuzi huo, mama ya mhasiriwa alimchuku na kwenda nyumbani kwao Mashuuru kabla ya kuripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Kimana.

Mdogo wa binti huyo akitoa ushahidi wake aliiambia mahakama jinsi siku hiyo mama yao akiwa kazini baba yao alifika nyumbani majira ya saa nane mchana akiwaamuru wote isipokuwa mlalamikaji aende kutafuta kuni.

Mvulana huyo alisema baada ya kurudi, hakukuwa na mtu nyumbani, hata hivyo wawili hao walirudi baadaye jioni.

Mshtakiwa alikamatwa akiwa katika Shule ya Wavulana ya Enkii ambako alikuwa akifanya kazi ya upishi mkuu na kusindikizwa hadi kituo cha polisi cha Loitoktok, ambako alishtakiwa kwa kosa hilo.

Mahakamani, mshtakiwa alikanusha madai hayo akisema ni ya kutunga. Hata hivyo, mahakama iliona upande wa mashtaka ulithibitisha kesi hiyo bila shaka, hivyo kutiwa hatiani na kutoa hukumu.

Mshtakiwa ana haki ya siku 14 ya kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.