Nyanya wa Junior Sagini, shangazi na binamu yake washtakiwa kwa kujaribu kuua

Washtakiwa hao walikana kutenda kosa hilo.

Muhtasari
  • Sagini sasa  yuko chini ya uangalizi wa maafisa wa Watoto na hali yake ya afya inaangaliwa na wataalam wa matibabu

Washukiwa watatu katika kesi ya mtoto Junior Sagini wamefikishwa katika mahakama ya Kisii na kushtakiwa kwa jaribio la kuua.

Alex Ochogo (Binamu ya Sagini), Pacifica Nyakerario (Shangazi) na Rael Nyakerario (nyanya) walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Christine Ogweno siku ya Ijumaa kufuatia kukamilika kwa uchunguzi wa polisi.

Watatu hao walishtakiwa kuwa kati ya tarehe 13 na 14 Desemba 2022 katika eneo la Ikuruma, Kaunti Ndogo ya Marani katika kaunti ya Kisii, walijaribu kinyume cha sheria kusababisha kifo cha Brighton Junior Sagini kwa kumng'oa macho yote mawili kinyume na kifungu cha 220 cha Sheria..

Washtakiwa hao walikana kutenda kosa hilo.

Wakili wa upande wa mashtaka, Hilary Kaino katika wasilisho lake aliiomba mahakama kuwanyima dhamana washtakiwa hao kwa madai kuwa wataingilia mashahidi ambao ni ndugu zao wa karibu.

"Napinga mahakama hii kuwapa washtakiwa dhamana kwa sababu wana uwezekano wa kuingilia mashahidi ambao ni ndugu zao wa karibu," alisema Kaino.

Kaino aliiambia mahakama kuwa kutoa dhamana au bondi kwa mshtakiwa kunaweza kuzua hofu, vitisho na wasiwasi hivyo kutokuwa na maslahi katika haki.

Kaino pia alipinga ombi la dhamana kutokana na utulivu, amani na usalama kwa wananchi kwa madai kuwa kesi hiyo ilivutia maslahi makubwa ya umma na kuna uwezekano wa washtakiwa kushambuliwa na wananchi kwa vile hali bado ni tete.

“Hizi ndizo sababu za msingi za mahakama hii kuwanyima bondi au dhamana,” alisema Kaino.

Wakili anayemtetea mvulana huyo mwenye umri wa miaka mitatu, Nduhukire Anita aliiambia mahakama kwamba anaungana na upande wa mashtaka kuwanyima washtakiwa dhamana.

“Kama upande unaohusika katika kesi hii, tunaiomba mahakama hii isiwaachilie washtakiwa kutokana na aina ya kesi, wanaweza pia kuingilia ushahidi na kuathiri shauri lililopo mahakamani,” alisema George Morara aliyekuwa akifuatilia muhtasari kwa serikali ya kaunti kama mhusika anayehusika.

Kwa sasa Sagini yuko chini ya uangalizi wa maofisa wa Watoto na hali yake ya afya inaangaliwa na wataalam wa matibabu.