Msichana wa chuo amchoma kisu mvulana mpenzi wake baada ya kumkataa kimapenzi

Msichana huyo alimtembelea mpenzi wake katika chumba chake bila kujua kuwa mvulana huyo alikuwa amemuandalia taarifa za kutamatisha mapenzi.

Muhtasari

• Msichana huyo alikuwa ameandamana na rafiki yake mwingine wa kike kwenda kwa mpenzi wake.

Mwanamke mjamzito apatikana amedungwa visu mgongoni
Mwanamke mjamzito apatikana amedungwa visu mgongoni
Image: Maktaba//The Star

Polisi katika kaunti ya Bomet wanamshikilia msichana mmoja mwenye umri wa miaka 21 anayetuhumiwa kwa kumdunga kisu mpenzi wake mvulana wa miaka 25.

Inadaiwa kwamba wanafunzi hao wapenzi ambao walikuwa wanasoma katika chuo cha Bomet walitofautiana baada ya mvulana kuamua kutamatisha mapenzi yao lakini msichana hakuwa anataka, jambo lililompelekea kumchoma kisu kifuani.

Polisi walinukuliwa na jarida moja la humu nchini kwamba msichana huyo alikwenda kumtembelea mpenzi wake katika nyumba yake akiwa ameandamana na rafiki yake wa kike wakati alipokezwa taarifa hizo na mpenzi wake mbele ya rafiki yake.

Akiwa amefadhaishwa na habari hiyo, msichana huyo alitoa kisu cha jikoni alichokuwa ameficha kwenye nguo zake za ndani na kumchoma. Rafiki yake alimzuia kabla hajamsababishia majeraha zaidi na akaomba usaidizi kutoka kwa wakaazi wa mtaa huo. Mpenzi huyo, ambaye alianguka baada ya shambulio hilo, alikimbizwa katika hospitali ya Tenwek akiwa hana fahamu, Nation waliripoti.

Msichana huyo alikamatwa na maafisa wa usalama wa shule na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Bomet kwa mahojiano.

Visa vya wanaume kushambuliwa Zaidi katika mahusiano ya mapenzi vimekithiri katika siku za hivi karibuni, huku makundi ya kutetea haki za kibinadamu yakitaka serikali pia kuchukua hatua kali dhidi ya wanawake watuhumiwa kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwa wanaume watuhumiwa.