Kasarani: Mrembo amwekea mwanamume dawa kwenye pombe, kisha kumuibia Ksh 849K

Baada ya kumfikisha kwake, mwanamume huyo aligutuka asubuhi bila simu, kadi 2 za ATM na kitambulisho.

Muhtasari

• Bw Sang alikuwa akifurahia vinywaji kwenye mkahawa mmoja na marafiki zake alipojumuika na mwanamke asiyemfahamu.

• Alipata taarifa za benki na kugundua kuwa Sh849,000 zilikuwa zimetolewa kutoka kwa akaunti yake ya benki. Pesa hizo zilitumwa kwa nambari tofauti za simu kupitia M-Pesa.

Mwanamke amwekea 'mchele' mwanamume kwenye baa kisha kumuibia 849k
Mwanamke amwekea 'mchele' mwanamume kwenye baa kisha kumuibia 849k
Image: Maktaba

Mwanamke mmoja anayedaiwa kumwekea dawa mtu katika baa mmoja huko Kasarani, Nairobi kabla ya kutoa Sh849,000 kutoka kwa akaunti zake tatu za benki baada ya kuiba simu yake alishtakiwa kwa kosa hilo.

Kwa mujibu wa ripoti zilizopo katika jarida la Nation, mwanamke huyo alimfanyia Fredrick Sang madhambi hayo Machi 12 kabla ya kumuibia pesa hizo pamoja na simu yenye thamani ya laki mbili na nusu.

Bw Sang alikuwa akifurahia vinywaji kwenye mkahawa mmoja na marafiki zake alipojumuika na mwanamke asiyemfahamu.

Baada ya kunywa kwa muda, Bw Sang aliondoka kwenye mkahawa huo na mwanamke huyo baada ya kumwomba ampeleke katika makazi yake katika mtaa wa Thome, Kasarani.

Mlalamishi aliamka siku iliyofuata na kujipata peke yake ndani ya gari lake lililoegeshwa katika kituo cha mafuta katika mtaa wa Thome. Mwanamke huyo alikuwa ametoweka, Nation waliripoti.

Simu zake mbili, kitambulisho cha taifa na kadi mbili za ATM pia hazikuwepo. Akaendelea na kazi. Wenzake walimjulisha kuwa simu zake zilikuwa zikiita bila kupokelewa.

Alipata taarifa za benki na kugundua kuwa Sh849,000 zilikuwa zimetolewa kutoka kwa akaunti yake ya benki. Pesa hizo zilitumwa kwa nambari tofauti za simu kupitia M-Pesa.

Baadaye Bw Sang alitafuta matibabu katika kliniki ambapo madaktari walimwambia kwamba vinywaji vyake vilikuwa vimewekwa dawa kwa kiwango kikubwa.

Baadaye aliripoti kisa hicho katika kituo cha Polisi cha Kasarani na idara ya Upelelezi wa Jinai ilichukua jukumu la uchunguzi.

Mwanamke ambaye alikuwa pamoja naye alifuatiliwa baadaye, akakamatwa na kushtakiwa kwa mashtaka yaleyale. Aliachiliwa kwa bondi ya Shilingi milioni 1.