Mahakama yaamuru Admin wa kundi la WhatsApp kumrudisha mwanachama aliyetolewa

Mlalamikaji aliiambia mahakama kwamba kundi hilo liliundwa kwa ajili ya michango na alipojaribu kujua kuhusu hesabu za fedha zilizochangishwa, Admin alimuondoa mara moja.

Muhtasari

• Mlalamikaji Baitwababo alisema, Asinguza alitengeneza kundi la Whatsapp kwa watu wa eneo la Buyanja ambalo lilikua na lengo la michango ya kijamii.

WhatsApp imo mbioni kuunda mfumo wa kuwezesha mtumiaji kutuma ujumbe kwa mtu bila kuwa na namba yake.
WhatsApp imo mbioni kuunda mfumo wa kuwezesha mtumiaji kutuma ujumbe kwa mtu bila kuwa na namba yake.
Image: Reuters

Mwanamume mmoja nchini Uganda amezua gumzo baada ya kuelekea mahakamani kuwashtaki waliomuondoa katika kundi la WhatsApp.

Kwa mujibu wa majarida ya nchini humo, Jumatatu wiki hii Hebert Baitwababo alielekea katika mahakama ya Mwanzo jijini Kampala akimshataki Admin wa kundi la WhasApp liitwalo Buyanja Roots, Allan Asinguza kwa kumtoa kwenye kundi hilo bila ya ridhaa yake.

Hakimu Igga Adiru alimtaka Asinguza kumrudisha mara moja Baitwababo kwenye kundi hilo.

Mlalamikaji Baitwababo alisema, Asinguza alitengeneza kundi la Whatsapp kwa watu wa eneo la Buyanja ambalo lilikua na lengo la michango ya kijamii na shughuli za kujitolea na kusaidiana kipindi cha majanga.

“Mimi kama mshirika wa kundi hilo, tulianzisha wazo la kutengeneza chama na tukakubaliana kutoa Shilingi 1760 kama ada mtu kujiunga na kuwa mwanachama, na mimi nilitoa ada hiyo ambapo taarifa zote za chama zilitolewa na kujadiliwa kupitia kundi hilo,” alisema Baitwababo katika hati za mahakamani.

Baitwababo alieleza kuwa Mei 16, 2023 akiwa mwanachama aliyesajiliwa wa chama hicho, alimwandikia barua Asinguza kutaka kujua kuhusu fedha zilizokusanywa kutoka kwa wanachama waliosajiliwa tangu mwaka wa 2017 lilipoanzishwa.

Alisema kwamba baada ya kumuandikia barua kiongozi huyo wa kundi ndipo alipoamua kumtoa kwenye kundi hilo mnamo Mei 17, 2023 ambapo kwa taratibu za kundi hilo, kuhoji michango ni kosa na ndipo Baitwababo alipoamua kutinga mahakamani kutoa malalamiko yake na mahakama kuamuru arudishwe.