Idara ya mahakama yalaani polisi kwa kuwashambulia wanahabari

Idara ya mahakama ilisema vyombo vya habari vinalindwa na Katiba, chini ya Kifungu cha 34 kuhusu Uhuru wa Vyombo vya Habari.

Muhtasari

• Mahakama ilisema inakumbatia uwazi, ushiriki wa raia na uwajibikaji katika kazi yake na kuongeza kuwa uwepo wa vyombo vya habari unasaidia katika kufanikisha hilo.

Benchi la majaji saba likiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome, naibu CJ Lady Justice Philomena Mwilu, Jaji Mohammed Ibrahim, Jaji Dkt. Smokin Wanjala, Lady Justice Njoki Ndungu, Jaji Isaac Lenaola na Jaji William Ouko wakati wa kongamano la kesi kabla ya kuanza kwa ombi la urais katika Mahakama ya Juu Agosti 30, 2022.
Image: DOUGLAS OKIDDY

Mahakama imelaani kunyanyaswa kwa wanahabari na maafisa wa polisi katika Mahakama ya Milimani siku ya Ijumaa.

Katika taarifa yake, Mahakama ilisema inakumbatia uwazi, ushiriki wa raia na uwajibikaji katika kazi yake na kuongeza kuwa uwepo wa vyombo vya habari unasaidia katika kufanikisha hilo.

"Tunalaani vikali unyanyasaji wowote wa wanahabari wanapotekeleza majukumu yao, popote na hasa ndani ya majengo ya mahakama," taarifa hiyo inasema.

Mahakama ilisema haizuii vyombo vya habari kuripoti kesi mahakamani isipokuwa wakati kuna sababu muhimu.

Idara ya mahakama ilisisitiza dhamira yake ya kudumisha uhuru wa vyombo vya habari, haki za wanahabari na utawala wa sheria.

Vyombo vya habari vinalindwa na Katiba, chini ya Kifungu cha 34 kuhusu Uhuru wa Vyombo vya Habari.

Mahakama ilitoa wito kwa kila kuonyesha viwango vya juu vya maadili katika majengo ya mahakama na ndani ya viunga vya mahakama.

“Mienendo ya wahusika wa kudumisha haki wakati  wote lazima wakuze na kuzingatia utawala wa sheria na kujenga imani ya wananchi katika mfumo wa utoaji haki,” idara hiyo ilikariri.

Kisa hicho kilitokea mapema Ijumaa wakati wanahabari waliokuwa wameenda katika mahakama za Milimani kuangazia uamuzi wa kuachiliwa kwa dhamana Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino waliposhambuliwa na maafisa wa polisi.