Mchungaji anayedaiwa kuingiza mikono kwenye nyeti za mwanamke wakati 'akimuombea' ashtakiwa

Mwanamke huyo alipatikana akivuja damu nyingi kwenye makalio baada ya pasta kudaiwa kuchomoa vipande vya nyama kutoka mwilini mwake.

Muhtasari

•Muriithi anadaiwa kumsababishia madhara makubwa ya mwili mwanamke huyo ambaye amekuwa akiugua kwa takriban miaka mitatu.

•Njiru alikamatwa nyumbani kwake mapema wiki hii alipokuwa akimuombea mwanamke huyo ambaye amekuwa akiugua kwa muda mrefu.

Mahakama
Mahakama
Image: MAHAKAMA

Mtumishi wa Mungu anayedaiwa kuingiza mikono yake kwenye sehemu za siri za ajuza mgonjwa wakati ‘akimuombea’ ameshtakiwa katika Mahakama ya Makadara.

Daniel Muriithi Njiru ambaye anaendesha kanisa la Only Believe Church of God Power of the Holy Spirit katika eneo la Mukuru kwa Njenga, jijini Nairobi anadaiwa kumsababishia madhara makubwa ya mwili muumini huyo wa umri wa miaka 62 ambaye amekuwa akiugua kwa takriban miaka mitatu.

Hata hivyo, alikanusha mashtaka mbele ya Hakimu Mkuu Irene Gichobi na kuachiliwa kwa bondi ya Sh100,000 au dhamana mbadala ya pesa taslimu Sh50,000. Hakimu aliamuru kesi hiyo kutajwa tena Septemba 6, huku kesi hiyo ikitarajiwa kuanza kusikilizwa Oktoba 30.

Upande wa mashtaka ulikuwa umekusanya mashahidi watano kutoa ushahidi dhidi ya mshtakiwa wakiwemo wanafamilia wa mwathiriwa, mwanachama wa nyumba kumi na maafisa wa polisi.

Njiru alikamatwa nyumbani kwake mapema wiki hii alipokuwa akimuombea mwanamke huyo ambaye amekuwa akiugua kwa muda mrefu.

Jumatano, Wakaazi wa mtaa wa mabanda wa Mukuru kwa Njenga Jwalimuokoa mwanamke huyo aliyekuwa mahututi kutoka kwa nyumba ya mshukiwa na kumpeleka katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta kwa matibabu.

Walisema walivutiwa na kilio cha muda mrefu cha mwanamke huyo na kuwaita polisi na wahudumu wa kujitolea wa afya ya jamii kumhudumia baada ya kushuhudia uchungu aliokuwa nao.

Wakazi walidai kuwa pasta huyo anayeendesha kanisa katika mtaa huo aliwaambia kwamba alikuwa huko kwa ajili ya 'maombi'.

"Kilichotokea hapa ni kitu ambacho hatujawahi kuona, tulishangaa sana na kujiuliza ikiwa Shakahola imekuja. Mchungaji alisema anamfanyia kujifungua," mkazi mmoja alisema.

Video iliyosambazwa mtandaoni inaonyesha mwanamke huyo akiwa amelala kitandani akiugua kana kwamba ana maumivu makali.

Majirani walisema kuwa mwanamke huyo alikuwa akivuja damu nyingi kwenye makalio baada ya kasisi huyo kudaiwa kuchomoa vipande vya nyama kutoka kwa mwili wake.

"Ilionekana zaidi kama uchawi, watu walipiga kelele na polisi wakaja na kumchukua hadi Kenyatta kuona kama angeweza kutibiwa. Hatujui kama atapona kwa sababu alikuwa ametokwa na damu nyingi."

"Damu ilikuwa ikitoka kwenye makalio kama maji na vipande vya nyama vilikuwa kwenye beseni," mkazi mwingine alisema.

"Baadaye tuligundua kuwa mwanamke huyu aliletwa hapa na bintiye kwa maombi baada ya mamake kuzunguka hospitali kadhaa na kuambiwa alihitaji kufanyiwa upasuaji."

Alisema mwanamke huyo alikuwa nyumbani kwa mchungaji huyo kwa wiki moja na Jumatano ilikuwa siku ya kuu ya maombi kwake.

"Hatujui tutaitaje hivyo kwa sababu hatujawahi kuona kitu kama hicho katika eneo hili.