Aliyekuwa mume wa Esther Arunga, Quincy Timberlake ahukumiwa miaka 11 jela kwa kifo cha mwanawe

Jaji Paul Freeburn alimfunga jela siku ya Ijumaa kwa kifo cha "kinyama na kisichoeleweka" cha mwanawe.

Muhtasari

•Sinclair mwenye umri wa miaka mitatu alikufa kwenye sakafu ya chumba cha kulala cha babake mjini Brisbane, Australia, mnamo Juni 2014.

•Mahakama ilisikia Timberlake alimpiga kwa nguvu tumboni, na kumfanya ajikwae, kisha akasema: "Kuna shetani tumboni mwake, ninamtoa pepo huyo tumboni mwake."

Esther Arunga na mumewe Quincy Timberlake. Picha/MAKTABA
Esther Arunga na mumewe Quincy Timberlake. Picha/MAKTABA

Mwimbaji mwenye utata Quincy Wambitta Timberlake mnamo siku ya  Ijumaa alihukumiwa kifungo cha miaka 11 nchini Australia kufuatia kesi yake ya kuua bila kukusudia kuhusu kifo cha mwanawe mnamo 2014.

Sinclair mwenye umri wa miaka mitatu alikufa kwenye sakafu ya chumba cha kulala cha babake mjini Brisbane, Australia, mnamo Juni 2014.

Timberlake alikiri kosa mwezi uliopita baada ya kuingia katika makubaliano ya kusihi na upande wa mashtaka, kwa adhabu ndogo.

Jaji Paul Freeburn alimfunga jela siku ya Ijumaa kwa kifo cha "kinyama na kisichoeleweka" cha mwanawe.

Timberlake alipata umaarufu nchini Kenya baada ya kufunga ndoa na aliyekuwa mtangazaji wa televisheni Esther Arunga mwaka wa 2010. Sasa wametengana.

Mwaka wa 2012, alitangaza kuwa angewania urais kupitia Chama chake kipya cha PlaCenta (Platinum Centraliser na Unionist Party of Kenya).

Hata hivyo, hakufanikiwa kuwania.

Siku ya Ijumaa, mahakama ilisikia kwamba baada ya kupata mwanawe akionekana ameanguka chini ya ngazi, Timberlake alianza kusema kwamba shetani alikuwa ndani ya nyumba, kulingana na Guardian.

Mwanaume huyo mbaye sasa ana umri wa miaka 43 alinyakua Biblia kutoka chumbani mwake, akisema angempiga shetani kofi, Jaji Paul Freeburn alisema katika kumhukumu Timberlake kwa kifo hicho "kikatili na kisichoeleweka".

Arunga alidhani mumewe alikuwa akishuka chini lakini akasikia mwanawe akipiga kelele na vishindo kutoka nyuma ya mlango wa bafuni alipotoka kuoga.

Mlango ulipofunguliwa, mvulana huyo alionekana kuwa na maumivu na ukaongezeka maradufu.

Mahakama ilisikia Timberlake alimpiga kwa nguvu tumboni, na kumfanya ajikwae, kisha akasema: "Kuna shetani tumboni mwake, ninamtoa pepo huyo tumboni mwake."

Sinclair alipoanza kumwendea mama yake, Timberlake kwa hasira alimrusha mtoto ukutani.

Baada ya mvulana huyo kuanguka chini, Timberlake alimwambia mke wake, "shetani ameenda sasa", kabla ya kujigamba kuhusu kumshinfa pepo huyo na kuliondoa kwenye tumbo la Sinclair.

Watoa huduma za dharura walipata mwili wa Sinclair kwenye sakafu ya chumba cha kulala.

Wanandoa hao walikosa  kuwaambia mamlaka kuhusu kile kilichotokea bafuni lakini Timberlake alirekodiwa kwa siri katika chumba cha kuhifadhia maiti akirejelea Biblia huku akiomba msamaha mara kwa mara kwa kumuangusha Sinclair.

Wiki kadhaa baada ya kifo hicho, Esther Timberlake - ambaye aliachiliwa mara moja kwa msamaha baada ya kukiri hatia mnamo 2019 ya kuwa msaidizi wa mauaji ya mwanawe - aliwaambia polisi kuhusu shambulio hilo, akisema mumewe alikuwa akipitia mambo yasiyokuwepo.

Baada ya kulazimishwa kuishi mitaani na kudhulumiwa akiwa mtoto, Timberlake alipata shahada ya uhandisi wa kemikali kabla ya kukutana na Esther, ambaye alikuwa amerejea Kenya baada ya kukubaliwa katika taaluma ya sheria nchini Australia.

Timberlake alikamatwa na kufungwa jela nchini Kenya, baada ya kutangaza nia yake ya kugombea urais baada ya wanandoa hao kuunda chama cha PlaCenta.