Mwizi wa watoto wachanga Kenya afungwa miaka 25 jela baada ya ufichuzi wa BBC

Alikamatwa mwaka wa 2020 kufuatia uchunguzi wa BBC AFRICA EYE na kupatikana na hatia mwezi uliopita.

Muhtasari

• Fred Leparan, ambaye alifanya kazi katika hospitali ya Mama Lucy Kibaki ya Nairobi, alirekodiwa akipokea $2,500 (£2,000) ili kumuuza mtoto wa kiume chini ya uangalizi wa hospitali hiyo.

Fred Leparan (kushoto) alipatikana na hatia baada ya kujaribu kumuuza mtoto wa kiume kwa mwandishi wa siri.
Fred Leparan (kushoto) alipatikana na hatia baada ya kujaribu kumuuza mtoto wa kiume kwa mwandishi wa siri.
Image: Brian Inganga/BBC

Mfanyakazi wa hospitali ya Kenya ambaye alifichuliwa na BBC akiuza mtoto kwenye masoko ya siri amehukumiwa kifungo cha miaka 25 jela.

Fred Leparan, ambaye alifanya kazi katika hospitali ya Mama Lucy Kibaki ya Nairobi, alirekodiwa akipokea $2,500 (£2,000) ili kumuuza mtoto wa kiume chini ya uangalizi wa hospitali hiyo.

Alikamatwa mwaka wa 2020 kufuatia uchunguzi wa BBC AFRICA EYE na kupatikana na hatia mwezi uliopita kwa ulanguzi wa watoto, kutelekeza watoto na kula njama ya kutenda uhalifu.

Mwandishi wa Africa Eye hapo awali alimjia Leparan akijifanya mnunuzi, baada ya kusikia kutoka kwa chanzo kwamba mfanyakazi mkuu wa kliniki ya kijamii alihusika katika ulanguzi haramu wa watoto kutoka hospitali inayosimamiwa na serikali.

Leparan alimuuliza mwandishi wa siri, ambaye alisema yeye na mumewe walikuwa na shida ya kupata mimba, maswali ya harakaharaka tu kuhusu hali yao kabla ya kukubali kumuuza mtoto wa kiume.

Siku ambayo mtoto huyo wa kiume na watoto wengine wawili walitakiwa kuhamishwa kutoka hospitali hadi kwenye makazi ya watoto ya serikali, Leparan alirekodiwa akidanganya hati za uhamisho ili makao hayo yatarajie watoto wawili, badala ya watatu.

Timu ya BBC ilihakikisha kwamba watoto wote watatu wamefikishwa moja kwa moja kwenye nyumba ya watoto, lakini walimrekodi Leparan akirekebisha makaratasi na kuwafahamisha kuwa mtoto huyo ni wao wa kumchukua.

Mahakama ya Kenya siku ya Jumatano ilisema Leparan atatumikia kifungo cha miaka 25 gerezani, kisha atatumia miaka 10 ya kipindi cha kuchunguzwa mienendo yake.