Naftali Kinuthia apatikana na hatia ya kumuua mwanafunzi wa chuo kikuu Ivy Wangechi

Wangechi aliuawa kwa kukatwakatwa kwa shoka nje ya Hospitali ya Rufaa ya Moi mjini Eldoret Aprili 9, 2019.

Muhtasari

•Familia ya marehemu na upande wa mashtaka wametaka hukumu ya juu zaidi kwa mauaji dhidi ya Kinuthia

Naftali Kinuthia na aliyekuwa mwanafunzi wa matibabu katika Chuo Kikuu cha Moi Ivy Wangechi Picha: FILE
Naftali Kinuthia na aliyekuwa mwanafunzi wa matibabu katika Chuo Kikuu cha Moi Ivy Wangechi Picha: FILE

Mahakama kuu mjini Eldoret imempata na hatia Naftali Kinuthia na hatia ya kumuua mwanafunzi wa chuo kikuu cha Moi Ivy Wangechi miaka minne iliyopita.

Hakimu Reuben Githinji alisema  kwamba upande wa mashtaka ulithibitisha kosa la mauaji na mshtakiwa atakumbana na sheria.

Hakimu alitupilia mbali utetezi wa Kinuthia ambapo mshtakiwa alidai alichokozwa na kuhamakishwa baada ya Ivy kukataa uhusiano wao wa kimapenzi na kuamua kutafuta mpenzi mwingine.

Jaji alibainisha kuwa ingawa Kinuthia alidai kwamba walikuwa na uhusiano wa karibu na marehemu hakuthibitisha hilo.

"Hata jumbe zilizokaguliwa hazikuthibitisha ushahidi wa uhusiano wa karibu na mshtakiwa pia hakuthibitisha uhusiano wa kimapenzi na marehemu," Githinji alisema.

Alibainisha kuwa mshtakiwa alitumia  shoka na kumpiga marehemu mara kadhaa na kumuacha bila uwezekano wa kuishi tena. 

Jaji alibainisha kuwa madai ya uchochezi ya Kinuthia hayakuwa ya kweli,Kinuthia alifuatilia kesi hiyo kwa njia ya video akiwa katika gereza la Eldoret  huku hakimu akiwa katika mahakama ya Malindi anakahudumu.

Familia ya marehemu na upande wa mashtaka wametaka hukumu ya kali zaidi kwa kosa la mauaji dhidi ya Kinuthia.

Wangechi aliuawa kwa kukatwakatwa kwa shoka nje ya Hospitali ya Rufaa ya Moi mjini Eldoret Aprili 9, 2019.

Kinuthia alisema alikuwa amesafiri hadi Eldoret siku hiyo ili kumtakia Ivy siku njema ya kuzaliwa ingawa uhusiano wao ulikuwa umeingia vumbi na kwamba alikuwa amezima simu yake na hivyo kushindwa kumfikia.

Mshukiwa  anasema alijaribu mara kadhaa kusuluhisha tofauti zao na kuwasiliana naye kupitia kwa rafiki aliyetambulika kama Mary Ann Chepkoech.

Alikuwa amemwomba Chepkoech amshawishi Ivy kwamba wakutane na kuzungumza .

Hapo awali alisema Ivy alikuwa amemjulisha kuhusu siku ya kuzaliwa na kwamba alihitaji Shilingi 28,000 ili kuandaa karamu.

Alimwomba amsaidie pesa hizo na Kinuthia akamtumia Shilingi 14,000 akiahidi kutoa salio mnamo Aprili 10 ambayo ilikuwa siku yake ya kuzaliwa.

Alisafiri hadi Eldoret kwa gari lake na kwenda kwa chuo cha matibabu ambapo aliegesha gari lake na kuamua kumtafuta Ivy ili wazungumze.

“Nilitaka kumtakia heri ya siku yake ya kuzaliwa na pia kumfahamisha kwamba singehudhuria sherehe hiyo kwa sababu nilipaswa kusafiri kurudi Nairobi  kufanya kazi," Kinuthia alisema.

Akiwa karibu na hosteli alimuona Ivy na kwenda kukutana naye. Ivy alishangaa kumuona na mara moja akamjulisha kuwa mpenzi wake mpya angegharamia sherehe ya kuzaliwa.

Alisema ilionekana wazi kuwa alikuwa amempuuza na hakutaka chochote naye.

"Katika mawazo yangu, nilihisi kama mtu aliyepotea na asiye na tumaini kwa sababu ya kile alichosema. Nilikasirika na kujisikia vibaya kwamba uhusiano tuliokuwa nao tangu 1998 ulikuwa umefikia kikomo ghafla," alisema.

Wakati huo nilirudi kwenye gari langu na niliamua sitazungumza naye tena. Akiwa anaingia kwenye gari alitazama nyuma na kumuona akiwa amekumbatiana na kushikana mikono na rafiki yake wa kiume umbali wa mita 50.

"Nilimuona  mwanaume aliyekuwa akimkumbatia  nilishindwa kujizuia, nilikuwa na hasira sana kwa sababu ya kile kilichokuwa kikifanyika mbele yangu. Siwezi kueleza vile niliamua kuchukua shoka na kumshambulia," alisema.

Alisema shoka hilo lilikuwa kwenye gari lake kwa zaidi ya mwaka mmoja na alilinunua kwa usalama wake kwa sababu ya kufanya kazi usiku mara nyingi.