Mahakama yaahirisha kutoa uamuzi wa kesi ya mauaji dhidi Maribe na Jowie

Iwapo watapatikana na hatia, adhabu ya Maribe na Jowie itakuwa hukumu ya kifo, ambayo mara nyingi huwa kifungo cha maisha

Muhtasari

• Wawili hao wamekuwa mahakamani tangu 2018, na upande wa mashtaka umeita mashahidi 35. Upande wa utetezi haukuita shahidi yeyote.

JELA AU UHURU?: Mwanahabari Jacque Maribe na Jowie Irungu katika mahakama ya Milimani mnamo Novemba 26, 2019. Picha: MAKTABA
JELA AU UHURU?: Mwanahabari Jacque Maribe na Jowie Irungu katika mahakama ya Milimani mnamo Novemba 26, 2019. Picha: MAKTABA

Mahakama Kuu kwa mara nyingine imeahirisha kutoa uamuzi katika kesi ambapo Joseph Irungu almaarufu Jowie na aliyekuwa mtangazaji wa televisheni Jacque Maribe wanashtakiwa kwa mauaji ya mfanyabiashara Monica Kimani. 

Jaji Grace Nzioka alisema Ijumaa kwamba atatoa uamuzi huo kufikia Machi 15, 2023. Mshtakiwa mkuu Jowie alikuwa mahakamani kwa ajili ya kutoa uamuzi huo huku mshtakiwa wa pili, mwanahabari Jacque Maribe akiripotiwa kuugua.

Wawili hao wanakabiliwa shtaka la mauaji. Serikali inadai wawili hao usiku wa Septemba 19, 2018, katika muda ambao haujajulikana katika Lamuria Gardens Apartment, Kitale Lane huko Kilimani jijini Nairobi, pamoja na wengine ambao hawakuwa mbele ya mahakama, walimuua mfanyibiashara Monica Kimani.

Mwili wake ulipatikana kwenye beseni la kuogea ukiwa umekatwa koo. Mikono na miguu yake ilikuwa imefungwa nyuma ya mgongo wake na mdomo wake ulikuwa umefungwa. Polisi walisema mauaji hayo yangehitaji zaidi ya mtu mmoja kutekeleza.

Kimani, 27, alihitimu diploma ya Uhusiano wa Kimataifa kutoka chuo cha Kenya Polytechnic. Alifanya mafunzo yake ya nyanjani katika Ubalozi wa Kenya huko Juba, Sudan Kusini. Wakati wa kifo chake, alikuwa akisimamia kampuni ya babake, MililePaul General Trading Company.

Mara kwa mara alisafiri hadi Juba na kurudi na kiasi kikubwa cha pesa kwa dola za Marekani. Kabla ya kuuawa alirudi na kiasi kikubwa cha fedha na alisimamishwa kwa muda kwenye uwanja wa ndege kwa sababu ya kubainisha alikokuwa amezitoa.

Alipiga simu kwa mtu mashuhuri na akaachiliwa. Hakuna rekodi ya tukio hilo. Alikuwa asafiri nje ya nchi muda mfupi na kumpigia simu rafiki yake Jowie.

Jowie alikuwa akifanya kazi kwa wanakandarasi wa kijeshi lakini pia hakuwa na kazi.

Wawili hao wamekuwa mahakamani tangu 2018, na upande wa mashtaka umeita mashahidi 35. Upande wa utetezi haukuita shahidi yeyote.

Mahakama hiyo inatarajiwa kutoa uamuzi wake leo (Januari 26).

Iwapo watapatikana na hatia, adhabu ya Maribe na Jowie itakuwa hukumu ya kifo, ambayo mara nyingi huwa kifungo cha maisha kwani hukumu ya mwisho ya kifo kutekelezwa nchini Kenya ilikuwa mwisho wa Julai 1987 baada ya jaribio la mapinduzi lililotibuka.

Mauaji ya Kimani yalishtua taifa hasa kwa sababu ya kukatwa koo. Ilileta shauku kubwa katika jamii.

Maribe wakati huo alikuwa amepandishwa cheo na kuwa mtangazaji mkuu wa habari wa Ijumaa katika runinga ya Citizen.

Uzito huo ulimfanya Jaji Wakiaga kutoa maagizo yanayomtaka Maribe kutosoma habari, kutoa maoni au kushiriki katika mahojiano yoyote moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na kesi ya mauaji.

Pia alisema Maribe hatasoma habari katika kipindi ambacho suala hilo limewekwa kwa ajili ya kusikilizwa.

Familia ya Kimani ilitaka wawili hao wahukumiwe wakiwa kizuizini. Kaka George Kimani aliapa hati ya kiapo akisema kuwa sababu ya mauaji ya marehemu haikujulikana na inawahatarisha zaidi kwani hawana uhakika kama uhalifu huo ulikuwa dhidi ya familia na huenda marehemu alikuwa tu mwathiriwa wa kwanza.

Katika utetezi wake, Jowie alikana kuhusika kwake na mauaji hayo. Aliambia mahakama kwamba suruali iliyokuwa na damu na ambayo imetumika kumhusisha na mauaji haikuwa yake. Suruali hiyo ni sehemu ya ushahidi wa mwendesha mashtaka.