Jowie alikuwa katika nyumba ya Monica Kimani mnamo siku ya kifo - Mahakama

Hakimu alisema kulikuwa na ushahidi wa kutosha kwamba Jowie alikuwa mtu wa mwisho kuonekana akiwa na Monica.

Muhtasari

• Mahakama imethibitisha kuwa Joseph 'Jowie' Irungu alikuwa katika nyumba ya Monica Kimani aliyeuawa mnamo siku ya kifo chake.

•Jowie alikuwa ameingia mahali alikoishi Monica kwa kutumia kitambulisho cha mtu mwingine.

katika Mahakama ya Milimani kabla ya hukumu ya mauaji ya mfanyabiashara Monica Kimani Februari 9, 2024.
Joseph Irungu almaarufu Jowie katika Mahakama ya Milimani kabla ya hukumu ya mauaji ya mfanyabiashara Monica Kimani Februari 9, 2024.
Image: DOUGLAS OKIDDY

Jaji Grace Nzioka sasa anasema mahakama imethibitisha kuwa Joseph 'Jowie' Irungu alikuwa katika nyumba ya Monica Kimani aliyeuawa mnamo siku ya kifo chake.

Hakimu alisema kulikuwa na ushahidi wa kutosha kwamba Jowie alikuwa mtu wa mwisho kuonekana akiwa na Monica katika nyumba yake ya Lamuria Gardens.

Jaji Nzioka alisema hilo lilithibitishwa na shahidi aliyelindwa ambaye pia alimtambua Jowie katika gwaride la utambulisho.

Jowie alikuwa ameingia mahali alikoishi Monica kwa kutumia kitambulisho cha mtu mwingine.

“Ni matokeo ya mahakama hii kuwa mshitakiwa wa kwanza alikuwa katika nyumba ya marehemu tarehe ya mauaji na alikuwa mtu wa mwisho kuonekana na marehemu, ushahidi wa shahidi mlinzi ni Harun ambaye alimtambua kwenye gwaride. kama mshitakiwa wa kwanza aliondoka kwenye nyumba hiyo saa tano usiku na hakuna mtu mwingine aliyekwenda kwenye nyumba hiyo," alisema.

"Ni ushahidi wa shahidi huyu kwamba mpenzi wa marehemu Monica kutoka Sudan hakuwepo Kenya. Na kuna ushahidi kwamba marehemu alitakiwa kusafiri siku iliyofuata kwenda Dubai kukutana na mpenziwe wa Sudan kwa biashara na likizo,"

Hukumu hiyo ilikuwa imeahirishwa mara mbili huku mara ya mwisho wakili wa Maribe, Katwa Kigen akiieleza mahakama kuwa alikuwa mgonjwa.

Jowie ndiye mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya Monica. Alishtakiwa pamoja na Jacque Maribe mnamo 2018.

Mwili wa Monica ulipatikana katika Ghorofa yake ya Lamuria Gardens ambayo iko Kitale Lane karibu na Barabara ya Denis Pritt huko Kilimani.

Wawili hao wamekuwa wakishtakiwa tangu 2018, na upande wa mashtaka umeita mashahidi 35.