Mkewe Wa Iria ashtakiwa kwa kesi ya ufisadi ya Sh351m

Jane Waigwe Kimani alishtakiwa pamoja na David Maina Kiama mbele ya hakimu wa mahakama ya Kupambana na Ufisadi Victor Wakumile.

Muhtasari
  • Jane alisema alikuwa mwathirika katika kesi hiyo kwa sababu ya uhusiano wake na mshtakiwa wa kwanza (Wa Iria) kwa uhusiano wa ndoa.
DAVID MAINA KIAMA NA MKEWE ALIYEKUWA GAVANA WA MURANG'A WA IRIA MBELE YA MAHAKAMA
Image: DOUGLAS OKIDDY

Mkewe aliyekuwa gavana wa Murang'a Mwangi wa Iria Jumanne alishtakiwa kwa kutoa kandarasi zisizo za kawaida za utoaji wa huduma za ununuzi wa vyombo vya habari za Sh351 milioni.

Jane Waigwe Kimani alishtakiwa pamoja na David Maina Kiama mbele ya hakimu wa mahakama ya Kupambana na Ufisadi Victor Wakumile.

Alikanusha mashtaka.

Jane na Kiama walishtakiwa huku wengine ambao tayari wameshtakiwa, walikula njama ya kutenda kosa la ufisadi kuhusiana na kandarasi isiyo halali ya utoaji wa huduma za ununuzi wa vyombo vya habari iliyotolewa kwa Top Image Media Consultants Limited na serikali ya kaunti ya Muranga ya jumla ya Sh351 milioni.

Kupitia kwa mawakili wao, washtakiwa waliiomba mahakama iwape masharti nafuu ya bondi.

Jane alisema alikuwa mwathirika katika kesi hiyo kwa sababu ya uhusiano wake na mshtakiwa wa kwanza (Wa Iria) kwa uhusiano wa ndoa.

Alisema hakuwa na hatia.

Kiama aliteta kuwa yeye ni wachache katika Top Image Media Consultants kwani tayari alikuwa amejiuzulu.

Hata hivyo, Upande wa Mashtaka uliitaka mahakama kuzingatia uzito wa kosa hilo kwani kiasi kikubwa cha fedha kinahusika.

"Madai kwamba Jane ni mwathirika katika kesi hiyo kwa sababu ya uhusiano wake na mshtakiwa wa kwanza sio kweli. Anashtakiwa kwa cheo chake kama mkurugenzi wa Kampuni ya Top Image Consultants", mwendesha mashtaka alisema.

Aidha, DPP aliiomba mahakama kuwapa washtakiwa hao masharti kwamba iwapo wataachiliwa wasiingilie mashahidi na pia waweke hati zao za kusafiria mahakamani.

Hakimu alizingatia mawasilisho ya upande wa utetezi na upande wa mashtaka.

Wawili hao waliachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh1 milioni au bondi ya Sh5 milioni na mdhamini wa kiasi sawa na hicho kila mmoja.

Mahakama ilibaini kuwa Kiama hana hati ya kusafiria lakini hafai kuondoka katika mamlaka ya mahakama.

Kesi hiyo itatajwa Mei 14.