Shahidi: Watuhumiwa wa kumchoma mwanamke kwa madai ya uchawi walikuwa ndugu zake

Mwelu alisema pia kulikuwa na jiwe kubwa sana kando ya Juliana

Muhtasari
  • Mtoto wa marehemu-Timothy Ngui alitoa ushahidi akisema washtakiwa walikuwa wakimwita mamake mchawi.
  • Chifu msaidizi aliambia mahakama kuwa washtakiwa wote walikuwa ndugu wa marehemu lakini alikuwa na uhakika hakuna damu mbaya kati yao.
Image: DOUGLAS OKIDDY

Watu wanne Alhamisi walifikishwa mbele ya mahakama ya Nairobi na kutoa maelezo kuhusu kisa ambapo mwanamke mmoja alichomwa hadi kufa katika kaunti ya Machakos miaka minne iliyopita kwa madai ya kufanya uchawi.

Kitongoji cha Misakwani, chifu msaidizi wa lokesheni ya Mumbuni Christine Mwelu aliambia mahakama kwamba aliupata mwili wa marehemu umechomwa moto.

“Tulipata kikosi cha zima moto kutoka kaunti ya Machakos tayari kimefika na kujaribu kuzima moto huo. Maafisa hao walipogeuza mwili wake, mikono na miguu yake ilikuwa imefungwa kwa waya. Ilionekana alikuwa amefungwa kabla ya nyumba kuchomwa moto," Mwelu alisema.

Mwelu alisema pia kulikuwa na jiwe kubwa sana kando ya Juliana

Chifu msaidizi aliambia mahakama kuwa washtakiwa wote walikuwa ndugu wa marehemu lakini alikuwa na uhakika hakuna damu mbaya kati yao.

Mtoto wa marehemu-Timothy Ngui alitoa ushahidi akisema washtakiwa walikuwa wakimwita mamake mchawi.

Mahakama ilisikia kwamba pia walipokea vitisho vya kuuawa ambavyo waliripoti katika kituo cha polisi cha Machakos kabla ya kuuawa.

Ngui alimweleza Hakimu Kanyi Kimondo kuwa washtakiwa walikuwa na nia ya kuwaangamiza familia nzima.

Usiku ambao mamake aliuawa, Ngui alisema mmoja wa washtakiwa alimpiga mamake mawe kabla ya kudaiwa kumchoma moto. Mwingine alimvamia kaka yake na kumkata, alivuja damu nyingi.

Maelezo ya kosa hilo ni kwamba mnamo Agosti 1, 2020, katika Kijiji cha Kathuma, kitongoji cha Misakwani, eneo la Mumbuni katika kaunti ndogo ya Machakos kaunti ya Machakos washtakiwa walimuua kwa pamoja Juliana Mwikali Ngui.

Shahidi mwingine Daniel Mutua ambaye ni mwalimu katika Shule ya Msingi ya Kyambuko huko Machakos aliambia mahakama kuwa anamfahamu marehemu. Alisema dada yake ameolewa katika boma hilo.

Mume wa dada huyo ni Anthony Mutua, mshtakiwa katika kesi ya mauaji.