Watu wawili washtakiwa kwa kutishia mbunge Ichung'wah na waziri Ndung'u

Wawili hao walishtakiwa mbele ya hakimu wa Milimani Rose Ndubi

Muhtasari

•Watu wawili walishtakiwa kwa kutishia kiongozi wa wengi Kimani Ichung'wah kupitia jumbe za whatsapp.

•Wawili hao aidha waliachiliwa kwa dhamana ya bondi ya ksh.100,000 baada ya kudaiwa kuwa  kipato chao ni cha chini.

Image: HISANI

Watu wawili wameshtakiwa kwa kutishia kumuua waziri wa hazina Prof. Njuguna Ndung’u na kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa, Kimani Ichung’wah, kutokana na swala tata la mswada wa fedha wa 2024/2025.

Washukiwa hao Stephen Mwangi Kamau na Kelvin Wafula Bwire walishtakiwa mbele ya hakimu wa Milimani Rose Ndubi. Walikanusha mashtaka ya kutuma jumbe za vitisho kwa wanasiasa hao wawili kupitia akaunti zao za kibinafsi za whatsApp.

Bwire alishtakiwa kuwa kupitia akaunti yake ya WhatsApp ijulikanayo kwa jina la @advokezadbiadboy na bila udhuru wa kisheria alituma ujumbe akisema;

“Wee mzee muda wako umekwisha na unapaswa kufa!” kwa CS Ndung’u.

Kamau alishtakiwa kwa kutuma ujumbe wa vitisho kwa Ichung’wah akisema: "Ninaapa ikiwa mswada utapita nitapanga ajali na hutapona".

Washtakiwa hao wawili walikabiliwa na mashtaka mengine manne ya kutumia lugha ya kashfa na dharau dhidi ya Ichung’wa na rais William Ruto.

Wakili wa utetezi aidha aliomba wawili hao kuachiliwa kwa dhamana

“Washukiwa hawa walikamatwa dhidi ya kupitishwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024/2025. Nchi nzima iko katika kimbunga hiki cha kuukataa Mswada huo."

Mahakama iliambiwa kuwa Kamau ni mpishi tu ambaye hupata Sh6,500 kutokana na ajira yake katika hoteli ya Nakuru na hawezi kumudu kiasi kikubwa cha bondi.

Upande wa mashtaka, hata hivyo, uliitaka mahakama kuweka dhamana ya juu kwa vile washtakiwa wametishia maisha ya wanasiasa hao wawili.

Hakimu aliambiwa kama alivyotabiri Kamau, afisi ya CDF ilibomolewa katika eneo bunge la Ichung’wah. Bi Ndubi alibatilisha upande wa mashtaka na kuwapa kila mmoja wa washukiwa hao dhamana ya pesa taslimu Sh100,000 akisema ni watu wa kiwango cha chini.

Wawili hao walifikishwa mahakamani siku moja baada ya maandamano ya siku ya Jumanne 25  kuhusu mswada tata wa fedha wa 2024/2025.