Washukiwa wa ufisadi kufikishwa mahakamani

Wanadaiwa kuiba mamilioni ya pesa katika mradi hewa wa barabara ya Thome - Tharua eneo bunge la Laikipia Mashariki

Muhtasari

• Aliyekuwa naibu kamishna jenerali wa magereza Benjamin Obuya  Njoga na washukiwa wengine 13 watafikishwa mahakani Milimani kujibu madai ya ufisadi.

• Wanadaiwa kupanga njama ya kulaghai idara ya serikali ya huduma ya kurekebisha tabia shilingi milioni 302.

Mahakama ya Makadara.
Mahakama ya Makadara.
Image: Maktaba

Arnold Karani na washukiwa wengine wanne wanatarajiwa kufikishwa katika mahakama ya kupambana na rushwa ya Nyahururu.

Watano hao wanashukiwa kupanga njama ya kupora fedha za mgao wa miradi ya kuimarisha eneo bunge la Laikipia Mashariki kutoka kwa serikali kuu.

Arnold Karani na wenzake wanatuhumiwa kupanga kutekeleza ubadhirifu ya shilingi milioni 19.2 zinazodaiwa kutumika katika ujenzi wa barabara ya Thome-Tharua.

Kulingana na tume ya kupambana na ufisadi (EACC), barabara hiyo haipo katika mwaka wa kifedha wa 2016/2017 katika eneo bunge la Laikipia Mashariki.

Wakati huo, katika mahakama ya kupambana na rushwa ya Milimani jijini Nairobi, washukiwa saba watafikishwa kortini kuanzia leo 16 Septemba 2024 hadi tarehe 19 Septemba 2024.

Saba hao wakiongozwa na Amos Kabue Mwangi wanakabiliwa na mashtaka ya ulaghai wa kufanya malipo kwa kwa bidhaa ambazo hazikusambazwa.

Mashtaka ya saba hao yanahusisha shilingi milioni 201.1 kutoka shule ya sheria ya Kenya kwa kampuni kadhaa ambazo hazikuwasilisha bidhaa wala kutoa huduma.

Mnamo Septemba 17,aliyekuwa naibu kamishna jenerali wa magereza Benjamin Obuya Njoga atafikishwa mahakama ya kupambana na hongo ya Milimani pamoja na washukiwa wengine 13.

Walishtakiwa na EACC kwa madai ya utumizi mbaya wa mamlaka, kumiliki mali ya umma kwa ulaghai na utakatishaji fedha.

Tuhuma za 14 hao zinahusu njama baina ya maafisa wakuu katika idara ya serikali ya huduma za marekebisho na wafanyabiashara kulagahai serikali shilingi milioni 302.