Magavana wa zamani kuhukumiwa mahakamani wiki hii

Aliyekuwa gavana wa Migori Okoth Obado na Mike Sonko wa Nairobi wanatarajiwa mahakamani katika kesi za ufisadi

Muhtasari

• Mike Sonko alishtakiwa kwa madai ya kufuja shilingi milioni 24.1 wakati akiwa gavana wa kaunti ya Nairobi pamoja na washirika wake kutoka kampuni moja ya kibinafsi.

• Zaidi ya shilingi milioni 500 zinatarajiwa kurejeshwa katika kesi inayomhusu aliyekuwa gavana wa Murang'a Mwani wa Iria zilizolipwa kwa zabuni iliyohsusha kampuni yake.

Mahakama ya Milimani jijini Nairobi
Mahakama ya Milimani jijini Nairobi

Waliokuwa magavana Mike Sonko wa Nairobi na Mwangi wa Iria wa Murang'a watahukumiwa katika mahakama ya kupambana na ufisadi ya Milimani jijini Nairobi tarehe 25 na 36 Septemba mtawalia.

Tume ya maadili na kupambana na rushwa  EACC iliwashtaki wawili hao kwa madai ya kuvuja rasilimali za umma kwa minajili ya kujifaidisha.

Mike Mbuvi Kioko Sonko maarufu kama Mike Sonko alishtakiwa pamoja na wengine watatu kwa madai ya kupeana zabuni kinyume cha sheria. 

Madai yanahusisha ufujaji wa shilingi milioni 24.1 kutoka kaunti ya Nairobi pamoja na wenzake kutoka kampuni moja ya kibinafsi.

Hukumu dhidi ya Sonko na wenzake itatolewa Jumatano tarehe 25.

Hukumu dhidi ya aliyekuwa gavana wa Murang'a Mwangi wa Iria, itasomwa mnamo tarehe 26.

Mwangi wa Iria pamoja na wengine walishtakiwa kwa madai ya kulipa shilingi milioni 547 kwa kampuni ya Top Image Consultants. Kampuni hiyo inahusishwa na gavana huyo wa zamani.

Katika kesi hiyo, EACC inalenga kurejeshwa kwa shilingi milioni 547 pamoja na vipande viwili vya shamba  vinavyodaiwa kuchukuliwa kwa njia za ufisadi.

Pia kesi dhidi ya aliyekuwa gavana wa Migori Okoth Obado itasikizwa tena tarehe 26 Septemba katika mahakama ya kesi za rushwa ya Milimani.

Obado pamoja na washukiwa wengine saba, walishtakiwa na kosa la kupanga njama ya kutekeleza  uhalifu wa kiuchumi.

Madai dhidi ya Obado yanahusisha matumizi mabaya ya shilingi milioni 74.5 kupitia wawakilishi alioteua katika miaka ya kifedha kuanzia mwaka wa 2013 hadi mwaka wa 2017.