Washukiwa wa utekaji nyara wa mwanablogu Chawa-001 wafikishwa mahakamani

Chawa alihadaiwa kuwa alikuwa anapelekwa kuomba radhi kwa gavana wa kaunti ya Mombasa

Muhtasari

• Mwanablogu alitekwa nyara nyumbani kwake na kutendewa unyama na watu kadhaa ambao baadaye walimuacha msituni akiwa bila fahamu.

• Washukiwa walikana mashtaka dhidi yao na sasa wamewekwa rumande katika jela ya Shimo la Tewa. Kesi yao itasikizwa mnamo tarehe 26 kubaini ikiwa wataachiliwa kwa dhamana.

Mfungwa akiwa jela
Mfungwa akiwa jela
Image: Mfungwa Jela

Kesi dhidi ya washukiwa wa utekaji nyara wa mwanablogu Bruce John Kajira maarufu kama Chawa 001, walifikishwa katika mahakama ya Shanzu kujibu mashataka dhidi yao mnamo Jumatatu 23, Septemba.

Washukiwa hao wanne waliotambulika kama Abdul Hassan Athman, Esther Muthoni,Violet Adera na Haji Babu Ndau Mohamed walikana mashtaka dhidi yao mbele ya mahakama ya sheria namba 4 ya Shanzu.

Taarifa za ujajusi zilizowasilishwa dhidi ya wanne hao mahakamani na maafisa wa DCI, zilisema kuwa washukiwa walitumia pikipiki yenye usajili KMFV 410G iliyopatikana na mshukiwa wa kwanza Abdul Hassan Athman.

Maafisa wa polisi wangali wanawatafuta washukiwa wengine wanaoaminika walihusika katika  utekaji wa Chawa 001 ambao pia walimbaka na kumlawiti mwathiriwa.

Ushahidi uliowasilishwa kortini ulisema kuwa wahalifu walikuwa na mawasiliano na wapangaji wa unyama huo ili kupewa mwelekeo na kufadhiliwa katika usafiri.

Washukiwa wanadaiwa kumhadaa Chawa 001 kuwa walikuwa wanampeleka kwa gavana wa kaunti ya Mombasa kuomba msamaha kwa chapisho la mtandao wa kijamii linalodaiwa kuwekwa na yeye akimtusi gavana wa Mombasa na familia yake.

Kisa hicho kiliripotiwa katika kituo cha polisi cha Bamburi baada ya mwathiriwa kusaidiwa na msamaria mwema aliyempata msituni.

Kulingana na marafiki wake wa karibu, Chawa 001 alipokea matibabu katika hospitali ya Beyond Scope Kisauni baada ya hospitali ya rufaa ya pwani kukataa kumpa huduma za matibabu.

Washukiwa hao walishtakiwa kwa makosa manne ya njama ya kutenda uhalifu, utekaji nyara, kulawiti na kumshambulia mathiriwa hadi kusababisha madhara ya mwili.

Hata hivyo walikana mashtaka dhidi yao.

Kesi dhidi ya wanne hao ilihairishwa na itatajwa tena mnamo Septemba 26, 2024 wakati mahakamaitaamua ikiwa wataachiliwa kwa dhamana.

Washukiwa wamewekwa rumande katika jela ya Shimo la Tewa.