
MAKACHERO kutoka katika idara ya upelelezi wa jinai, DCI wamewakamata washukiwa ambao wamekuwa wakiwazawadi wakenya katika kaunti ya Mombasa shahada za uzamili na uzamivu baada ya mafunzo ya siku tatu tu.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye akaunti yao ya X mnamo
Februari 13, 2025, DCI ilifichua kwamba watu hao walikuwa wakiendesha shughuli
zao katika chuo kikuu cha muda kilichoanzishwa katika Kaunti ya Mombasa.
Washukiwa hao wanne ni pamoja na Wakenya 2, Mmarekani mmoja
na Mpakistani mmoja ambao walikuwa wanatoa mafunzo ya siku 3 kwa watu katika
hoteli moja kisha kuwatunuku PhD na Masters.
“Raia wawili wa kigeni ni
miongoni mwa washukiwa wanne ambao wametiwa mbaroni katika oparesheni kali
inayolenga chuo kikuu cha simu ambacho kilikuwa kimepewa makao kwa muda katika
hoteli moja kaunti ya Mombasa. Wanne hao walipatikana wakitoa Shahada za
Uzamili na Uzamivu kwa washiriki waliochangamka waliokuwa wamepata mafunzo kwa
siku tatu pekee,” DCI ilitaarifu.
Wanne hao walikamatwa na maafisa wa kutekeleza sheria kutoka
Kituo cha Polisi cha Bamburi, baada ya kupata taarifa kuhusu shughuli za
kutisha za kundi hilo.
Baadhi ya shahada zilizotunukiwa kwa njia ya udanganyifu ni
pamoja na Shahada tatu za Uzamili ya Utawala wa Biashara (Uongozi na
Menejimenti) na Shahada za Uzamivu mbili za Uongozi.
Watuhumiwa hao wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya
Sheria ya Shanzu ambapo walisomewa shitaka la Kutoa Shahada Bila Ithibati ya
Vyuo Vikuu vya Nje Kinyume na Kifungu cha 28(2) kikisomwa na kifungu cha 5 cha
Sheria ya Vyuo Vikuu, DCI iliarifu.
Washtakiwa hao walikana hatia ambapo walipewa dhamana ya Ksh
400,000 na mdhamini sawa na lazima wafanyike kwa kiapo mbele ya mahakama ya
wajibu au dhamana ya pesa taslimu ya Ksh 300,000.
Pasipoti za wageni hao wawili pia ziliwekwa mahakamani na
kutajwa kupangwa tarehe 18 Februari, 2025.
“DCI inaonya kuwa hakuna
juhudi zitasalia katika kuwakamata washukiwa wanaotoa vyeti kwa njia ya ulaghai
kwa watu ambao wanashindwa kutoa jasho,” ripoti ilisema.
Mnamo Aprili 2024, Rais William Ruto alifichua kuwa zaidi ya
watu 2,100 walio na vyeti ghushi vya masomo walikuwa wakifanyia kazi serikali.
Wakati huo, Ruto aliamuru walio na vyeti vya ulaghai kuacha
nyadhifa za serikali na kutafuta kulipwa pesa walizochuma kimakosa kutoka kwa
serikali.
“Sasa tutakabiliana na janga la ufisadi moja kwa moja, iwe ni
katika kaunti, iwe katika serikali ya kitaifa. Hebu fikiria, ukaguzi rahisi wa
watu wanaofanya kazi serikalini umefichua kuwa tuna watu 2,100 walio na vyeti
ghushi (vya kitaaluma) wanaofanya kazi serikalini,” Ruto alisema.