HIV:Imani potofu ambazo bado zipo mwaka 2021

Muhtasari
  • Alipogundulika kuwa na Virusi vya Ukimwi, mnamo 1988, ilibidi aache mafunzo ya uuguzi

Mara ya mwisho Paul Thorn alipowaona wazazi wake, miongo kadhaa iliyopita, walitupa sahani alizotumia kula kwa kuhofia kuambukizwa.

Alipogundulika kuwa na Virusi vya Ukimwi, mnamo 1988, ilibidi aache mafunzo ya uuguzi.

"Niliishi miaka yangu yote ya 20 kwa hofu," anasema. Sasa, Bw Thorn, aliye nchini Uingereza, hafikirii kuhusu virusi hivyo - mbali na kumeza kidonge kwa siku na kumtembelea daktari wake mara mbili kwa mwaka.

Watu walio na Virusi vya Ukimwi wanaopokea matibabu wanaweza kufurahia maisha ya kawaida kabisa - na fikra zilizopitwa na wakati na zisizo sahihi kwamba virusi - vinaweza kupatikana kutokana na kushirikiana sahani moja mara nyingi zimetoweka - lakini habari potofu bado zinasambazwa.

'Kuna tiba'

Doreen Moraa Moracha, kutoka Kenya, alizaliwa na Virusi vya Ukimwi lakini aligundua akiwa na umri wa miaka 13, mwaka wa 2005.

Tangazo la televisheni lilimpeleka kwa mwanaume mmoja nchini Tanzania, aliyedai kuwa mganga, ambaye alisema anaweza kumponya Bi Moraa Moracha na mama yake.

"Tulikunywa dawa za mitishamba ambazo alikuwa akiuza na tukarudi tukiamini kuwa hatuna VVU," alisema.

Aliacha kutumia dawa zake za kupunguza makali ya virusi, ambazo huzuia virusi kujirudia - hadi akashikwa na vipele na homa ya mapafu kwa sababu ya mfumo wake wa kinga dhaifu.

Na wingi wa virusi vyake - ni kiasi gani cha VVU kwenye damu - kilikuwa juu sana daktari wake alimwambia ikiwa angepata maambukizi mengine, yangemuua.

Ikiwa haijatibiwa, VVU inaweza kusababisha ugonjwa wa upungufu wa kinga (Ukimwi) - ugonjwa ambao mwili hauwezi kupigana hata na maambukizi madogo.

Madai ya tiba ni ya kawaida, rais wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ukimwi Dk Adeeba Kamarulzaman anasema. Lakini hakuna chanjo au tiba ya VVU.

Visa vya hivi karibuni vya watu kupona virusi vimeongeza matumaini.

Mwezi huu, mwanamke nchini Argentina alikua mtu wa pili aliyethibitishwa kuwa hana VVU kwa njia ya mfumo wake wa kinga. Lakini haijaeleweka ni kwa jinsi gani au kwa nini.

'Utaambukiza kila wakati'

Joyce Mensah - ambaye anatoka Ghana lakini alihamia Ujerumani kuepuka unyanyapaa - anasema amepoteza mahusiano na hata kazi yake kwa sababu ya imani potofu kuhusu hali yake.

Unyanyapaa unatokana na udanganyifu kwamba watu wenye VVU daima wako katika hatari ya kueneza kwa wenzi wao au mtoto, anasema.

"Mtu anapofichua hali yake ya VVU kwa mwanafamilia au mshirika... watu wana dhana hii potofu kwamba si salama kwa 100%, mara tu unapoambukizwa, unakuwa na VVU," Bi Mensah anasema. Kwa hakika, baada ya kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU kwa muda wa kutosha, watu hawatapitisha virusi kwa vile hakuna maambukizi yanayoweza kupimika ya kusambaza (ingawa bado watakuwa na VVU na watahitaji matibabu ya maisha yote).

Bi Mensah alikuwa na watoto wanne alipokuwa kwenye matibabu - na hakuna aliyepata virusi.

Ulimwenguni kote, maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yamepungua kwa nusu tangu 2010, kwani matibabu yameenea zaidi.

Lakini nchini Ghana, binti wa Bi Mensah hivi karibuni alirudishwa nyumbani kutoka shuleni kwake kwa imani potofu kwamba yeye pia alikuwa na virusi - na angeweza kuwaambukiza wengine.

Ian Green, Mtendaji Mkuu wa Shirika la misaada la Uingereza Terrence Higgins Trust, ambaye anaishi na VVU, alisema: "Suala kubwa zaidi kwa watu wanaoishi na VVU, na hakika uzoefu wangu pia, mara nyingi unajiona kama msambazaji magonjwa.

''Kwa miaka mingi, nilikuwa na hofu kuhusu kusambaza virusi kwa mtu mwingine. "Kujua sasa kwamba haiwezekani kwangu kusambaza virusi, hiyo imekuwa ukombozi mkubwa."

'HIV imekwisha'

VVU sio hukumu ya kifo tena na watu walio na virusi wanaweza kuishi maisha ya kawaida na yenye afya, baadhi ya wanaharakati wanasema mitazamo imebadilika sana.

"Kumekuwa na maendeleo ya kushangaza katika matibabu na zana za kuzuia VVU lakini mtazamo huu kwamba Ukimwi umekwisha, katika suala la kuzuia - sio muhimu sana, na kwa hakika katika suala la kuwekeza katika kutafuta tiba ya VVU," Dk Kamarulzaman anasema.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha mwaka 2020, takriban watu milioni 38 duniani kote walikuwa wanaishi na VVU na 700,000 walikufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na Ukimwi, ambayo yanaweza kuwa matokeo ya virusi kutotibiwa.

Bw. Thorn anasema vijana huona kama ugonjwa wa wazee, Bw. Green anaunga mkono hilo, ambaye anasema wana "kwa ujumla hawana uelewa". "Wanafikiri kwamba VVU ni kitu cha zamani," anaongeza.

'Mimi sio aina ya mtu ambaye nitapata VVU'

Jinsi vijana wanavyoona ni ugonjwa wa watu wazima, wengi huona virusi hivyo kuwa ni jambo linaloathiri wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja pekee.

Duniani kote, zaidi ya nusu ya watu walio na VVU ni wanawake - na ndio huua wanawake walio katika umri wa kuzaa, kwa mujibu wa Christine Stegling, wa shirika la misaada la Frontline Aids.

Lakini wanawake wachache anaozungumza nao wanajua hatari yao.

"Ni data muhimu sana kujihusisha nayo, kwa sababu wanawake walio katika rika hilo na wanawake ambao wanaweza kutaka kuwa wajawazito wanapaswa kuwa na mazungumzo kuhusu ngono isiyo salama," Bi Stegling anasema.

Ingawa maendeleo makubwa yamepatikana, habari potofu ambazo bado zinasambazwa zinaweza kuwaacha watu bila kazi, uhusiano, matibabu sahihi au hata utambuzi wa ugonjwa huo.