Jinsi mfanyikazi katika kiwanda cha chuma cha Thika alivyochemka hadi kifo, jino peke lilibaki

Muhtasari

•Alipotupa  vipande vya chuma ndani, glavu zake zilikwama kwenye vyuma hivyo na kufanya avutwe kwenye mashine ambayo iliyomponda vipande vipande kabla ya kumwangusha kwenye tanuru la moto.

•Wafanyakazi wenzake wa Otieno walisema, ingawa tukio hilo la kusikitisha lilikuwa la kwanza, majeraha mabaya katika kituo hicho ni ya kawaida, na kutilia shaka viwango vya usalama pale

Marehemu Calleb Otieno
Marehemu Calleb Otieno
Image: JOHN KAMAU

Kila mara Caleb Otieno alishirikiana na mfanyakazi mwenzake ambaye alibadilishana naye zamu ili kupata chakula cha mchana.

Ijumaa iliyopita, alimpa mwenzake Sh50 ili amletee chakula cha mchana kiwandani. Hata hivyo, mwenzako aliporudi na chakula, Otieno hakuwepo tena.

Alikuwa ameagiza ugali na mchanganyiko wa mboga,minji zilizochemshwa na maharagwe.

Otieno alikuwa na jukumu la kupitisha vipande vya chuma hadi kwenye tanuru la moto.

Wakati akitupa vipande vya chuma ndani, glavu zake zilikwama kwenye vyuma hivyo kufanya avutwe kwenye mashine ambayo iliyomponda vipande vipande kabla ya kumwangusha kwenye tanuru la moto.

Mikono na kichwa chake vilikuwa vya kwanza kupondwa. Kisha mwili wake uliokuwa umeyeyuka ukachanganyika na chuma kilichoyeyuka, na kuacha chembe nyingi tu za mfupa kwenye msingi.

Tukio hilo la kutisha liliacha woga na simanzi miongoni mwa wafanyakazi wenzake, huku hata wakishindwa la kufanya, ikiwa ni pamoja mahali pa kupeleka chakula chake.

Otieno, 34, anatoka Kogony mjini Kisumu. Alifika jijini baada ya kumaliza masomo yake ya kidato cha 4 katika Shule ya Upili ya Kisumu Day miaka 10 iliyopita.

Alianza kufanya kazi kama mfanyakazi wa kawaida katika Bidco Africa kabla ya fursa kuja kubisha hodi katika Kampuni ya Blue Nile Rolling Mills, ambapo alifanya kazi kwa miaka saba hadi kifo chake cha kusikitisha.

DCIO wa kaunti ndogo ya Thika Joseph Thuvi alisema kuwa walitembelea kituo hicho Jumapili na kukusanya majivu na chembechembe zilizoonekana kama vipande vya mifupa kutoka kwenye tanuru.

Thuvi alisema wanachukulia suala hilo kama ajali ya kawaida mahali pa kazi.

Wakurugenzi wa kampuni hiyo na afisa wa rasilimali watu walitembelea ofisi ya DCI Jumatatu na Jumanne asubuhi kama sehemu ya uchunguzi.

Majivu ya Otieno yamehifadhiwa katika mochari ya General Kago yakingoja uchunguzi wa maiti.

"Tutafanya uchunguzi wa maiti familia ikiwa tayari na itakapotaka kufanya maziko, nasubiri waniambie," Thuvi alisema.

Kulingana na Rose Nyambura ambaye anauza chakula katika kibanda kilicho kwenye lango la kiwanda hicho, marehemu alikuwa mteja mcheshi na wa kawaida ambaye alitimiza ahadi zake.

Nyambura alisema kila mara Otieno alipochukua chakula kwa mkopo, alilipa kama alivyoahidi.

Baadhi ya wafanyakazi wenzake wa Otieno walisema, ingawa tukio hilo la kusikitisha lilikuwa la kwanza, majeraha mabaya katika kituo hicho ni ya kawaida, na kutilia shaka viwango vya usalama pale.

Madai ya wafanyakazi hao yalithibitishwa na wachuuzi wa chakula waliokuwa kwenye lango la kiwanda hicho.

"Ni malalamiko ya mara kwa mara miongoni mwao [wafanyakazi]. Najua kwa sababu wanakula hapa," Nyambura alisema.

Jitihada nyingi za gazeti la Star kutaka uongozi wa kiwanda hicho utoe ufafanuzi juu ya tuhuma hizo au kutoa mwanga kuhusu mazingira ya matukio hayo ziligonga ukuta na walinzi na vyombo waliagizwa kutoruhusu watu kuingia.

Pia walikataa kuzungumza juu ya suala hilo kwa simu