Wazee wachapwa viboko katika Makao ya Wazee ya PCEA Thogoto, Kiambu

Makao hayo ya wazee ni nyumbani kwa takriban wanawake 50 wazee na wanaume.

Muhtasari

•Upigaji picha wa siri unaonyesha wafanyikazi wakiwatesa wakazi, wakitupa chakula moja kwa moja kwenye meza bila sahani yoyote, na kuwaacha bila matibabu.

•Mfanyikazi mmoja anaonekana akimchapa mwanamke huyo mzee kwenye makalio yake kwa kutumia fimbo ya mbao.

Image: BBC

Wakazi walio katika mazingira magumu katika makao ya wazee karibu na mji mkuu Kenya, Nairobi wamekuwa wakinyanyaswa na kutelekezwa, uchunguzi wa BBC Africa Eye umefichua.

Upigaji picha wa siri unaonyesha wafanyikazi wakiwatesa wakazi, wakitupa chakula moja kwa moja kwenye meza bila sahani yoyote, na kuwaacha bila matibabu.

"Mchape katika makalio. Mpige," mfanyikazi mmoja anamsihi mfanyakazi mwenzake aliyeshika fimbo, katika Kanisa la Presbyterian Church of East Africa (PCEA) Thogoto Care Home for the Aged, takriban kilomita 20 (maili 12) magharibi mwa Nairobi.

Picha za siri zinaonyesha kwamba muda mfupi kabla, wafanyakazi watatu waliovalia sare za rangi ya zambarau, wanamzingira mwanamke mzee karibu na lango la chuma lililozungukwa na mabati pembezoni mwa bustani ya nyumba hiyo.

"Ulikuwa unaelekea wapi upande huo?" anauliza mmoja wa wafanyakazi. "Uliitwa ukakataa kurudi."

Ajuza huyo aliyevalia kofia, anaonekana kuchanganyikiwa na kuogopa.

"Oh, tafadhali nisamehe," anasema.

"Sasa inabidi tukuchape," anasema mmoja wa wafanyakazi.

Mfanyikazi mmoja anaonekana akimchapa mwanamke huyo mzee kwenye makalio yake kwa kutumia fimbo ya mbao.

Huu ni mfano mmoja tu wa ushahidi wa unyanyasaji uliofichuliwa katika uchunguzi wa BBC Africa Eye.

Nyumba ya kuwatunza wazee hao ilianzishwa na Chama cha Wanawake cha kanisa la ndani la PCEA lakini sasa inajitegemea. Ni nyumbani kwa takriban wanawake 50 wazee na wanaume.

Katika muongo uliopita, idadi ya nyumba za wazee inaripotiwa kuongezeka mara tatu zaidi jijini Nairobi. Wengi hawatozi kodi na hutegemea makanisa ya ndani au michango.

Katika miaka 30 ijayo idadi ya wazee barani Afrika inakadiriwa kuongezeka mara tatu kutoka milioni 75 hadi milioni 235, kulingana na ripoti ya Ofisi ya Sensa ya Marekani ya 2020.

Ukuaji wake utakuwa wa haraka zaidi kuliko katika eneo lingine lolote la ulimwengu, na kufanya uwezekano wa kuwapeleka waliozeeka kwenye makao ya kuwatunza kuwa jambo halisi kwa idadi kubwa ya familia zonazoongezeka.