Nyota wa YouTube wa Marekani aibua hisia tofauti baada ya kutangaza kuwa alijenga visima barani Afrika

Baadhi ya Waafrika wamemkosoa, wakisema kuwa video yake inaendeleza dhana ya Afrika kama bara masikini.

Muhtasari

•Bw Beast amepokea sifa na kukosolewa baada ya kuwashirikisha wafuasi wake taarifa kwamba alijenga visima 100 barani Afrika.

Image: BBC

Nyota wa YouTube wa Marekani na mhisani Bw Beast amepokea sifa na kukosolewa baada ya kuwashirikisha wafuasi wake taarifa kwamba alijenga visima 100 barani Afrika.

Katika video hiyo, ambayo imetazamwa zaidi ya mara milioni 48 tangu kutolewa kwake Jumamosi, Bw Beast alionyesha ujenzi wake wa visima 52 katika jamii za mashambani za Kenya na visima vingine 48 katika nchi za Zimbabwe, Uganda, Somalia na Cameroon.

Watu kadhaa wamempongeza Bw Beast kwa kusaidia jamii za mashambani, huku wakizilaumu serikali za Afrika kwa ubadhirifu wa fedha zilizokusudiwa kwa miradi kwa utekelezaji wa miradi hiyo.

Bw Beast, ambaye jina lake halisi ni Jimmy Donaldson, ana watumiaji milioni 207 kwenye YouTube, na hivyo kkuifanya akaunti yake kuwa akaunti inayofuatiliwa zaidi kwenye jukwaa hilo.

"Najua ni ajabu kwamba MwanaYouTube lazima afanye mambo haya yote, lakini lazima mtu afanye. Na ikiwa hakuna mtu mwingine, tutafanya hivyo. Inabadilisha sana maisha ya jamii tunazozijenga,” Bw Beast alisema kuhusu msukumo wake wa mradi huo.

Lakini baadhi ya Waafrika wamemkosoa, wakisema kuwa video yake inaendeleza dhana ya Afrika kama bara masikini.

Wengine wameibua wasiwasi juu ya athari za kimazingira za visima hivyo, wakisema vinaweza kuchangia katika kupunguza maji ya ardhini.

Bw Beast ametetea msaada wake akisema kuwa atatumia jukwaa lake kila mara kusaidia watu na kuwatia moyo wengine kufanya vivyo hivyo.