Kinywa kinaashiria nini kuhusu afya ya miili yetu?

Afya ya kinywa chako inaweza kuwa kiashirio rahisi na sahihi cha kile kinachotokea katika mwili wako wote.

Muhtasari

•Ugonjwa wa fizi, au periodontitis, kama "maambukizi makubwa ya ufizi ambayo huathiri tishu laini zinazozunguka meno.

•Ni muhimu kwamba watu wanaweza kufikia mfumo mzuri wa afya ya kinywa, na kwamba watu wawe na daktari wa meno wanayemwamini 

Image: BBC

Unapokwenda kwa daktari wa meno, huwa unafikiria tu kuhusu kutunza meno yako, ukikisahau kabisa kinywa chako.

Lakini unaweza kukosa taarifa muhimu ukifanya hivyo: afya ya kinywa chako inaweza kuwa kiashirio rahisi na sahihi cha kile kinachotokea katika mwili wako wote.

Zaidi ya hayo, kudumisha afya nzuri ya kinywa ni muhimu linapokuja suala la kuweka mwili wako katika hali bora.

"Kuna baadhi ya matangazo" nchini Uingereza, alisema Profesa Nikos Donos, mkurugenzi wa utafiti katika Taasisi ya Madaktari wa Meno katika Chuo Kikuu cha Queen Mary cha London wakati wa jopo la kwenye makala ya The Evidence ya BBC, "ambapo wanauliza: 'Je! unaweza kulipuuza jicho linalotoka damu?Kwa nini unapuuza fizi wakati linapotoa damu?'

"Na bado, kuna watu ambao wanapitia maisha na ugonjwa mbaya wa fizi na wanaamini kuwa ni kawaida."

Kuna ushahidi wa kutosha unaohusisha hasa ugonjwa wa fizi au periodontitis na ugonjwa wa kisukari na ugonjwa wa moyo, na kuna tafiti zaidi na zaidi zinazothibitisha kwamba afya bora ya kinywa inaweza kuwa mojawapo ya vita vinavyopuuzwa zaidi katika mapambano dhidi ya magonjwa haya.

"Tunapozungumza kuhusu uhusiano kati ya magonjwa sugu tofauti na sehemu nyingine za mwili na kinywa, tunaona kuwa kuna kuenea kwa ugonjwa wa fizi," Donos alielezea.

"Na tunaona kwamba ugonjwa wa fizi ni ugonjwa wa sita unaojulikana zaidi kwa wanadamu, unaopatikana kwa karibu kwa watu bilioni 1.1, 11.2% ya idadi ya watu."

Ugonjwa wa fizi

Kliniki ya Mayo nchini Marekani inafafanua ugonjwa wa fizi, au periodontitis, kama "maambukizi makubwa ya ufizi ambayo huathiri tishu laini zinazozunguka meno.

Bila matibabu, periodontitis inaweza kuharibu mfupa unaoshikilia meno yako." na kuyafanya kulegea au kuanguka.

Miongoni mwa dalili zinazowezekana ni ufizi unaovuja damu, uwekundu au maumivu au harufu mbaya inayoendelea kutoka.

Lakini zaidi ya uharibifu unaoweza kusababisha kinywa chako, kuna ushahidi wa kutosha unaounganisha ugonjwa wa fizi na kisukari cha aina ya 2.

"Kwa kweli, kwa sasa tunazungumzia uhusiano wa pande mbili," Donos alisema, "ambayo ina maana kwamba wagonjwa wa periodontal wako katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kisukari na wagonjwa wa kisukari pia watakuwa na ugonjwa wa periodontal."

Uhusiano huo ni wa karibu kiasi kwamba kuna tafiti zinazothibitisha kwamba huduma nzuri ya kinywa kwa watu wenye kisukari cha aina ya 2 inaweza kusaidia kudhibiti ugonjwa huo kwa ujumla, kwa njia rahisi na bila madhara makubwa.

"Utafiti tuliofanya miaka michache iliyopita ulionesha kuwa ikiwa unatibu ugonjwa wa periodontal kwa kawaida bila uingiliaji wa upasuaji kunakuwa na udhibiti bora wa kimetaboliki kwa wagonjwa hawa, uboreshaji mkubwa ambao ulidumishwa kwa karibu miezi 12," Donos alisema.

Pia aliyeshiriki katika jopo la BBC alikuwa Dk. Graham Lloyd Jones, mtaalamu wa radiolojia katika Hospitali ya Salisbury nchini Uingereza, ambaye alihakikisha kwamba uhusiano kati ya kinywa na kisukari "una maana."

"Lazima tuone kinywa kama kiungo cha kinga ya mwili : ikiwa umeathiriwa, kutakuwa na michakato ya uchochezi, ikiwa ni pamoja na pathogens, bakteria ambao kwa kawaida huishi kwenye kinywa lakini hupita kwenye sehemu nyingine za mwili ambazo zinahusika katika maendeleo na kutokea kwa mengi ya magonjwa haya,” daktari alionya.

Kutoka kinywani mpaka kwenye moyo

Image: BBC

Aina ya 2 ya kisukari sio ugonjwa pekee unaohusiana na ugonjwa wa fizi: kwa sababu bakteria wasiodhibitiwa wa periodontitis husafiri kupitia mwili kupitia mfumo wa damu, wanaweza kuishia kuathiri moyo.

"Sehemu hizi za uchochezi ambazo zipo katika mwili kutokana na ugonjwa wa periodontitis na ambazo hufika kwenye damu," Donos alisema, "zinaweza kuunda 'utando' ambao unaweza kusababisha kuganda kwa damu ambayo inaweza kuwa na matokeo kwa wagonjwa kuanzia matatizo ya moyo wa ischemic hadi mashambulizi ya moyo."

Kesi ya maambukizi ambayo yanaweza kusababisha kifo na ambayo hutokea wakati ulinzi wa kinywa ni mdogo, kutokana na ugonjwa wa kinga au matumizi ya madawa ya kulevya.

"Kwa bahati nzuri ni ugonjwa adimu," anaeleza Dk Lloyd-Jones, "lakini ni ugonjwa wa kuambukiza ambapo baadhi ya viumbe katika kinywa hutoka nje ya udhibiti na kuathiri tishu za ndani ya moyo."

"Ni dhahiri kwamba njia hii ya anatomiki ya kinywa, yenye vimelea vya magonjwa ambayo huenda kwenye mwili wote, ni kitu halisi.

Baada ya muda, ziada hii ya bakteria ambayo huvuka kizuizi cha kimwili cha kinywa chetu hufikia mwili wote kupitia kijito cha damu, ambayo inaweza kusababisha magonjwa.

Uhusiano na hali ya utambuzi

Image: BBC

Ingawa ushahidi sio thabiti kama katika kesi zilizopita, kuna watafiti wengine ambao wanaanza kufichua nini kinaweza kuwa uhusiano kati ya bakteria hawa na kupungua kwa hali ya utambuzi katika uzee.

Mmoja wao ni Dk Vivan Shaw, kutoka Chuo Kikuu cha Cambridge, ambaye alithibitisha katika utafiti wake amegundua kuwa watu wanaofikia uzee na meno 21 au zaidi wana kuzorota kwa utambuzi kuliko wale ambao wana meno machache.

"Ingawa ushahidi ni wa hivi karibuni, tunaweza kusema kwamba ikiwa una aina fulani ya uharibifu wa utambuzi na kupoteza ustadi, uwezo wako wa kusafisha meno au kunyoosha meno yako unaweza kuathirika," Shaw anasema.

"Pia inahusiana na suala la lishe: ikiwa una meno machache, hakika utakuwa na lishe mbaya zaidi, ambayo husababisha hali kuzorota zaidi."

Lloyd-Jones, kwa upande wake, alizungumzia kiungo cha moja kwa moja: "Kuna viumbe maalumu ambavyo vimehusishwa na maendeleo na kuongezeka kwa ugonjwa wa fizi."

''Kiumbe mahususi, kinachojulikana kama gingivalis, ni kiumbe kinachovutia sana. Imefunikwa na neurotoxins, ambayo huua seli. Lakini kiumbe hicho hakibaki tu mdomoni, huacha ufizi wetu uliovimba na kusafiri mwilini, na hupatikana katika ubongo na ugiligili wa ubongo wa watu walio na ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.

Kwa Profesa Donos, mahusiano haya kati ya kinywa na mifumo tofauti ya mwili yanaonesha tu umuhimu wa kuzuia ugonjwa wa periodontal.

Utunzaji wa kinywa

Image: BBC

"Magonjwa yote ya kinywa yanazuilika na kwa kiasi fulani, yanatibika - isipokuwa saratani, ambayo ni hadithi tofauti kabisa," Donos alisema wakati wa jopo.

Kwa mtaalamu, ni muhimu kwamba watu wanaweza kufikia mfumo mzuri wa afya ya kinywa, na kwamba watu wawe na daktari wa meno wanayemwamini ambaye ana uwezo wa kuzingatia kinga.

"Hiyo ndiyo njia ya kusonga mbele. Na pia unganisha udaktari wa meno na dawa kwa ukaribu zaidi, ili tunapomtembelea daktari wetu, daktari wetu wa meno, wasiangalie meno yetu au ini letu tu, bali waone mwili kama mfumo; na kuoanisha dalili."

Mfano mahususi ambapo mchanganyiko huu wa utaalamu unaweza kufanya kazi ni katika utunzaji wa ujauzito: Dk. Shaw alisema kutokana na mabadiliko ya homoni yanayotokea wakati wa ujauzito, bakteria hao wa kinywani wanaweza kupata nguvu na kuwaweka kinamama na mama na watoto katika hatari.

"Tuna wasiwasi sana kwa sababu huongeza hatari ya kuzaliwa kabla ya wakati na kuzaliwa kwa uzito wa chini, ndiyo maana ni hatua muhimu kuzungumza na mama na kuwapa huduma ya kutosha."

Kwa Lloyd-Jones, sehemu muhimu zaidi ni kubadili jinsi tunavyofikiri kuhusu vinywa vyetu: “ Ni lazima tufikirie wazo hilo la kinywa chetu kuwa kizuizi cha kinga ambacho huhitaji utunzaji . Tunza vijidudu muhimu vinavyoishi kwenye vinywa vyetu na ambavyo vipo kwa ajili ya kutulinda.