Kwa nini Kanisa la Katoliki haliko tayari kutambua ndoa za wapenzi wa jinsia moja

Mnamo Desemba 18, Papa Francis alipendekeza kwamba makasisi waruhusiwe kuwabariki wapenzi wa jinsia moja

Muhtasari

•Vatican ilitangaza kwamba mapadre wanapaswa kuruhusiwa kubariki wapenzi wa jinsia moja na "wasio wa kawaida" chini ya hali fulani.

•Tangazo la Desemba 18 limemweka rafiki wa kibinafsi wa Papa chini ya uangalizi - Kardinali Victor Fernandez.

Image: BBC

Tangazo kwamba Papa Francis amewaruhusu makasisi kuwabariki wapenzi wa jinsia moja ni maendeleo makubwa kwa watu wa LGBT+ katika Kanisa Katoliki la Roma.

Lakini wataalam wanasema kwamba uamuzi huo si lazima uwe ni maendeleo makubwa ya Vatican kuelekea kutambua ndoa za wapenzi wa jinsia moja.

Katika hati iliyoidhinishwa na papa na iliyotolewa tarehe 18 Disemba, Vatican ilitangaza kwamba mapadre wanapaswa kuruhusiwa kubariki wapenzi wa jinsia moja na "wasio wa kawaida" chini ya hali fulani.

Hata hivyo, andiko hilo lilisema kwamba baraka hizo hazipaswi kuwa sehemu ya taratibu za kawaida za Kanisa. Vatican inaendelea kuiona ndoa kuwa muungano kati ya mwanamume na mwanamke. Kulingana na Filipe Domingues, profesa katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian huko Roma:

"Kuchapishwa kwa waraka huo ni jambo muhimu sana kwa sababu watu hawakutarajia tangazo rasmi [kutoka Vatican]," Prof Domingues alisema.

Lakini mtaalam huyo anadokeza kwamba hakuna dalili dhahiri kwamba Kanisa linanuia kuchukua hatua zaidi kuelekea kukubali ndoa za wapenzi wa jinsia moja .

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Wataalamu wanasema hati iliyoidhinishwa na Papa Francis na iliyotolewa tarehe 18 Disemba haionyeshi dalili zozote kwamba Kanisa linakusudia kuchukua hatua zaidi za kukubali ndoa za watu wa jinsia moja.

"Katika hati hiyo kuna uthibitisho wa sakramenti ya ndoa ni nini na mapitio ya maana ya baraka. Hili liko wazi sana."

Taarifa ya awali ya Vatican kuhusu suala hilo iliyochapishwa mwaka 2021, ilipinga baraka za ndoa za watu wa jinsia moja kwa hoja kwamba Mungu “hawezi kubariki dhambi”.

"Papa hakuridhika sana na toleo la mwisho la waraka wa 2021. Licha ya hayo, alitoa idhini," Profesa Domingues aliongeza, akibainisha kuwa tangu wakati huo Papa Francis ametoa sauti ya upatanisho zaidi.

Baraka za kila aina

Kanisa Katoliki lina aina kadhaa za baraka. Kulingana na sheria za ibada ya hadhara, Mkatoliki lazima “apate kupatana na mapenzi ya Mungu yanayoonyeshwa katika mafundisho ya Kanisa” ili kupokea baraka.

Lakini Papa Francis sasa ameanzisha uelewa zaidi wa kichungaji au wa kijamii kuhusu baraka.

Hati ya tarehe 18 Desemba inasema kwamba yeyote anayeomba kubarikiwa "anajionyesha akihitaji uwepo wa wokovu wa Mungu" na anafanya "ombi la msaada kutoka kwa Mungu, ombi la maisha bora".

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Wakristo wanaotaka kuoa mtu wa jinsia zao wanaweza kupokea baraka chini ya baadhi ya makanisa.

"Waraka huo unaweka wazi kabisa kwamba baraka hiyo mpya haifai kufanywa kuwa jambo la kawaida. Inapaswa kufanywa kwa njia isiyo rasmi, ya papo hapo, bila kutumia neno ndoa au kuwa na tambiko maalum," alieleza Prof Domingues.

"Ni hatua ya vitendo kusaidia watu katika hali ambayo wanahisi wapo nje au mbali na Kanisa."

Mapadre wanaweza kukataa

Kwa namna fulani, hii ilikuwa tayari inafanyika katika parokia za Kikatoliki za Kirumi chini ya mashauri ya ndani ya baadhi ya mapadre au maaskofu. Kuanzia sasa na kuendelea, kuna kile mwanasosholojia Francisco Ribeiro Neto, mtaalamu wa kidini katika Chuo Kikuu cha Sao Paulo, nchini Brazili, anachokiita uhalalishaji wa kitaasisi.

"Baraka hii ya asili ya uchungaji ilikuwa tayari kutolewa. Sasa kuna kichocheo, uthibitisho kutoka Vatican kwamba ishara hii ya kukaribishwa inayotamaniwa na Kanisa," anasema Ribeiro Neto.

"Lakini padre halazimiki kutoa baraka, anaweza kutathmini msingi wa tukio katika uhalisia wake. Kanisa linasema ni kwamba waamini wana haki ya kupata huduma ya kichungaji."

Mwanasosholojia huyo pia anaamini kuwa tangazo la Desemba 18 haliwezi kuonekana kama hatua ya kukubalika kwa ndoa za wapenzi wa jinsia moja na Kanisa Katoliki la Roma.

"Papa Francis hasogei kuiruhusu lakini badala yake anaunda kategoria ambayo inahakikisha kukubalika kwa wapenzi wa jinsia moja, bila kuleta baraka inayotolewa kwa ndoa za jinsia moja," anasema.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Kadinali Fernandez (kulia) aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika moja ya nyadhifa muhimu zaidi katika Kiti Kitakatifu

Ribeiro Neto anaona hatua hii kama njia ya kutuliza sekta zote za mila na desturi za kisasa za Kanisa.

"Inamaanisha kwamba anaunda kikundi [katika jaribio] la kukomesha utata huu kuhusu kukubali au kutokubali ndoa za wapenzi wa jinsia moja ambao wanataka kutambuliwa na Kanisa na kupata baraka hii."

Ribeiro Neto, hata hivyo, anasisitiza kwamba baraka haimaanishi kwamba Kanisa limeidhinisha uhusiano huo.

Rafiki wa Papa wa Argentina

Tangazo la Desemba 18 limemweka rafiki wa kibinafsi wa Papa chini ya uangalizi - Kardinali Victor Fernandez. Kasisi huyo wa Argentina aliteuliwa hivi majuzi katika taasisi ya Dicastery for the Doctrine of the Faith - moja ya idara kongwe za utawala za Kanisa. Anajulikana pia kwa maoni ya mtazamo wa kisasa na yenye utata.

Fernandez, kwa mfano, ndiye mwandishi wa vitabu kadhaa, ikiwa ni pamoja na kimoja ambacho anawahimiza wanandoa kufanya mazoezi ya busu za kimapenzi. Hajawahi kukwepa kushughulikia hadharani maswala yenye utata kama vile kukaribisha wanandoa katika ndoa ya pili na kukuza msimamo wa kirafiki zaidi kwa maswala ya LGBT.