Jinsi mchungaji TB Joshua alivyoficha kuporomoka kwa jengo la Lagos

Kuporomoka kwa jengo hilo ni mojawapo ya maafa mabaya kuwahi kutokea katika eneo la ibada barani Afrika.

Muhtasari

• TB Joshua alificha maiti na kuzitisha familia ili kuficha jukumu lake katika kuporomoka kwa jengo ambalo liliua takriban watu 116 katika kanisa lake mnamo 2014.

•Walioshuhudia walisema TB Joshua alikuwa ameonywa kuhusu matatizo ya kimuundo kabla ya maafa hayo. Wanasema maelezo ya ndege yalikuwa "uongo".

B Joshua (juu) siku zote alisema kuanguka kwa jengo kulisababishwa na ndege ya ajabu
B Joshua (juu) siku zote alisema kuanguka kwa jengo kulisababishwa na ndege ya ajabu
Image: BBC

BBC imegundua ushahidi mpya kwamba kiongozi wa kanisa kuu la Nigeria marehemu TB Joshua alificha maiti na kuzitisha familia ili kuficha jukumu lake katika kuporomoka kwa jengo ambalo liliua takriban watu 116 katika kanisa lake mnamo 2014.

Kuporomoka kwa jengo hilo ni mojawapo ya maafa mabaya kuwahi kutokea katika eneo la ibada barani Afrika.

Uchunguzi wa BBC ni mara ya kwanza kwa watu wa ndani wa Kanisa la TB Joshua la Synagogue Church of All Nations (Scoan) mjini Lagos kuwasilisha ushahidi wa kilichosababisha tukio hilo takriban miaka 10 iliyopita, na jinsi mchungaji huyo anadaiwa kupanga kuficha ukweli.

Inafuatia ushahidi uliofichuliwa na BBC wa unyanyasaji na utesaji ulioenea na mwanzilishi wa mojawapo ya makanisa makubwa zaidi ya kiinjili ya Kikristo duniani.

Siku mbili baada ya kuanguka kwa jengo hilo tarehe 12 Septemba 2014, TB Joshua alisema hadharani kuwa mkasa huo ulikuwa na na uhusiano na ndege iliyopita juu ya jengo lililokuwa likitumiwa kuhifadhi mahujaji wanaozuru.

Lakini uchunguzi uliofanywa na mchunguzi wa maiti wa Lagos ulikubaliana na wafanyakazi wa dharura kwamba kushindwa kwa kimuundo kulisababisha nyumba ya wageni kuanguka, na kusema ilikuwa imejengwa bila ruhusa ya idara ya mipango ya ujenzi.

Walioshuhudia waliambia BBC kwamba TB Joshua alikuwa ameonywa kuhusu matatizo makubwa ya kimuundo kabla ya maafa hayo. Wanasema maelezo ya ndege yalikuwa "uongo".

"Alijua kuwa jengo hilo lilikuwa dhaifu," anasema Emmanuel, ambaye alihudumu zaidi ya muongo mmoja kama mfuasi wa TB Joshua - kikundi cha wafuasi wachamungu waliokuwa wakiishi katika kanisa lake huko Lagos.

Kama wanafunzi wengi wa zamani waliohojiwa na BBC, alichagua kutumia jina lake la kwanza pekee.

Alieleza mchungaji huyo akipokea taarifa, saa chache kabla ya kuporomoka, kwamba jengo hilo lilikuwa "linayumba" na "linatetemeka".

Mashahidi wengi wanasema wageni hawakuonywa. Badala yake zaidi ya 200 kati yao waliongozwa kwenye chumba cha kulia cha jengo hilo kwenye ghorofa ya chini kula chakula chao cha mchana - ambapo walikuwa wameketi wakati ghorofa zote sita za saruji zilishuka juu yao.

Wengi waliuawa papo hapo, lakini zaidi ya 100 walinaswa ndani wakiwa hai.

"Nilisikia watu wakilia: 'Nisaidie, nisaidie, nisaidie," anasema Emmanuel, ambaye alikuwa kwenye eneo la tukio ndani ya dakika chache baada ya kuanguka.

"Sauti zao zilikuwa zikififia na unaweza kusema kuwa watu hawa wanakufa."

Wengine walielezea waathiriwa waliojeruhiwa vibaya, na macho na miguu iliyopotea - iliyogawanywa na mihimili iliyoshuka juu yao.

"Ilikuwa wazi kwamba jengo hilo halikujengwa kwa urefu ambao TB Joshua alijenga," anasema Rae, kutoka Uingereza, ambaye alikuwa akiishi kwa miaka 12 kanisani kama mfuasi.

Anasema alikuwepo wakati TB Joshua alipowaamuru wafanyakazi wake kujenga ghorofa za ziada: "Misingi haikujengwa kushikilia jengo la ghorofa nyingi kiasi hicho.

"Aliendelea tu kusukuma na kusema: 'Naitaka juu zaidi. Ni lazima iende juu zaidi. Ni lazima iende juu zaidi."

Wadadisi wa mambo ya kanisa waliozungumza na BBC pia wanasema maisha yangeweza kuokolewa iwapo TB Joshua angejibu mara moja kuporomoka kwenyewe. Badala yake, wanasema, alizuia huduma za dharura kufikiaeneo la mkasa kwa saa 24 - madai yaliyothibitishwa na ripoti za habari wakati huo .

Wakati wa kipindi hiki muhimu cha kuokoa watu na kusaidia waliojeruhiwa, mashahidi wa BBC wanasema baadhi ya wafanyakazi wa kanisa walijaribu kuokoa maisha kwa njia za kizembe na zisizo za kawaida. Bila kutumia vifaa vya kiufundi au mafunzo ya matibabu, walitumia zana kutoka kwa idara ya matengenezo ya kanisa.

Katika tukio moja, mfanyakazi wa kanisa alidaiwa kutumia msumeno kumkata mguu mwanamume aliyekuwa amenaswa chini ya vifusi.

"Alikuwa akipiga kelele!" Anasema Emmanuel, akionekana kutikiswa wakati wa mahojiano yake. Hana uhakika kama mtu huyo alinusurika.

"Niliona mambo mengi ambayo yalinitia kiwewe sana… nyuso zilipondwa," asema Michael, mfuasi ambaye alikuwa yungali bado kijana wakati huo.

Shuhuda za watu waliojionea matukio hayo ya kutisha hazijawahi kuchapishwa hapo awali, huku watu wengi wa ndani ya kanisa wakiapa kuficha, na eneo la mkasa likikingwa kutoka kwa watu kwa ukuta mkubwa.

Vyanzo vitatu, akiwemo Michael, vinasema TB Joshua aliamuru wafanyakazi wake kuhamisha milundo ya maiti mbali na eneo la jengo lilipoporomoka wakati wa usiku, ili kuzificha kutoka kwa vyombo vya habari na mamlaka.

CHANZO CHA PICHA,PIUS UTOMI EKPEI

Maelezo ya picha,

Wafanyikazi rasmi wa dharura waliripotiwa kuzuiwa kutoka kwa eneo la kuanguka kwa masaa 24

Wawili wanasema walitakiwa kurekodi shughuli hii, na kuwasilisha kanda hizo kwa TB Joshua ofisini kwake.

"Tulikuwa tukizirekodi huku zikiweka kwenye mifuko ya miili... mirundo ya miili ya watu," anasema Michael.

Chloe, mfuasi wa zamani wa TB Joshua kutoka Uingereza, pia alishuhudia matukio ya baada ya kuporomoka kwa jengo hilo. Anasema aliingia kwenye basi na mara moja aliona harufu mbaya.

Dereva alimwambia gari lilikuwa "limejaa maiti ... na tunawasafirisha usiku ili waandishi wa habari wasiweze kuwaona".

Vyanzo vingi vinaamini kuwa idadi ya waliokufa ilikuwa kubwa kuliko ile ya 116 iliyotolewa na kanisa, na kutaja marafiki na wafanyikazi wa kanisa ambao walikuwa ndani wakati wa kuanguka kwa jengo ambao wanasema hawakurekodiwa katika orodha rasmi ya waliokufa.

Awali mamlaka ya Nigeria ilichukua msimamo mkali kuhusu maafa hayo. Mchunguzi wa maiti wa Lagos alipendekeza kuwa TB Joshua ashtakiwe kwa uzembe wa uhalifu.

Licha ya kuitwa mara nyingi, TB Joshua hakuwahi kuhudhuria kikao cha kortini.

Baadhi ya wanafunzi wake wa zamani wanasema alitoa pesa nyingi kwa watu wenye ushawishi juu ya kesi katika kipindi hiki. Hii ilijumuisha maelfu ya dola za kimarekani, randi za Afrika Kusini na naira za Nigeria kwa familia za wahanga wa jengo hilo, 85 kati yao wakitoka Afrika Kusini.

Sihle, mfuasi wa zamani wa TB Joshua, aliiambia BBC kuwa alipewa kazi hii nchini Afrika Kusini "kwenda kutoa pesa, mifuko ya pesa" kwa wale waliopoteza jamaa.

"Tungewaambia wasizungumze na vyombo vya habari, wasitoe ripoti au chochote. Kimsingi, tulikuwa tunawanyamazisha," anasema.

Maelezo ya picha,

Llwandle Mkhulisi wa Afrika Kusini anashikilia kuwa alipewa "pesa za damu" kwa dada yake Pumzile, ambaye alikufa katika ajali hiyo.

Familia tatu nchini Afrika Kusini zilithibitisha kwa BBC kwamba wawakilishi wa kanisa walijaribu kuwapa pesa na kuwakatisha tamaa kuzungumza na waandishi wa habari.

Llwandle Mkhulisi, kutoka Johannesburg, ambaye alipoteza dada yake Pumzile katika maafa hayo, alizitaja fedha hizo kuwa ni "pesa za damu" na kuzikataa.

Baada ya kupokea zawadi ya awali kutoka kwa kanisa ya randi 50,000 (kama dola 2,500; £2,000), Sonny Madzhiye kutoka Benoni karibu na Johannesburg anasema alikataa mabunda ya fedha yaliyofuata baada ya kifo cha binti yake Sibongile.

Anasema alianza kugundua kuwa alikuwa akipewa pesa hizo ili asichukue hatua zaidi. TB Joshua alimsumbua kwa simu baada ya kuzikataa na kumtishia: "Alinitumia jumbe hizi. Inasema: 'Ikiwa utazingatia kile ulichopoteza, unaweza kupoteza kila kitu.'

"Sasa ananitishia kuwa familia yangu yote itaangamia, jinsi binti yangu alivyoshuka."

Alionyesha jumbe hizi na rekodi ya simu kutoka kwa TB Joshua .

Baadaye Bi Madzhiye amejaribu kuishtaki Scoan katika mahakama ya kiraia nchini Nigeria, akitaka fidia kwa kifo cha binti yake. Kesi inaendelea.

Sihle anasema waandishi wa habari pia walipewa fedha baada ya maafa, ili kushawishi utoaji wao wa taarifa.

"Tungekuwa na waandishi wa habari wanaokuja kanisani kwa jambo moja au lingine, lakini waandishi wa habari wangeondoka na bahasha… angetoa kwa dola," anasema.

Chloe, ambaye alifanya kazi katika idara ya waandishi wa habari ya TB Joshua, alithibitisha kuwa waandishi wengi walipewa pesa katika kipindi hiki. Hii ilithibitishwa na wanahabari wawili waliozungumza na BBC na openDemocracy - mshirika katika uchunguzi huu.

Katika rekodi ya siri iliyofanywa na mwandishi wa habari wa Nigeria Nicholas Ibekwe mnamo Septemba 2014, TB Joshua anaweza kusikika akisema: "Sasa utaandika nini?" baada ya kutoa pesa kwa wanahabari waliojaa meza kutumia bahasha za pesa. Ibekwe alikataa ofa ya pesa taslimu.

Maelezo ya picha,

Sonny Madzhiye anasema bado anasubiri haki kwa kifo cha bintiye

Emmanuel na Michael, ambao kila mmoja alihudumu zaidi ya miaka 20 ndani ya kanisa hilo, wanasema waliamrishwa na TB Joshua kuweka bahasha za pesa kwenye magari ya wanasiasa wa Nigeria na maofisa wa mahakama wakati wa uchunguzi wa maiti wa Lagos.

"Alifunika kila kitu," anasema Emmanuel. "Alinunua mfumo mzima."

TB Joshua alifariki Juni 2021, akiwa na umri wa miaka 57, lakini kanisa hilo sasa linaendeshwa na mjane wake Evelyn.

BBC iliwasiliana na Scoan na madai hayo katika uchunguzi wetu. Haikuwajibu, lakini ilikanusha madai ya awali dhidi ya TB Joshua.

"Kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Nabii TB Joshua si jambo geni... Hakuna madai yoyote yaliyowahi kuthibitishwa," iliandika.

Hadi leo, wanachama wengi wa Scoan wanaamini kwamba ndege ya ajabu ndiyo iliyosababisha kuporomoka kwa jengo hilo. Video zinazotoa dai hili, zinazotolewa na kanisa hilo, zimetangazwa kwenye chaneli yao ya satelaiti ya Emmanuel TV kote ulimwenguni na inasambazwa sana kwenye YouTube.

Chloe, ambaye alihudumu miaka 14 kama mfuasi wa TB Joshua, anaamini "familia [za waathiriwa] zilipata dhuluma kubwa".

Karibu muongo mmoja baadaye, hakuna mtu aliyewahi kufunguliwa mashitaka kwa kuanguka kwa jengo hilo. Nyumba ya wageni ya zamani, umbali mfupi kutoka ukumbi mkuu, bado ina uharibifu.

"Sikujua nilikuwa nikimtuma binti yangu kanisani ili auawe," asema Bi Madzhiye, akilia katika mahojiano yake na BBC. Bado anahifadhi chumba cha bintiye kama alivyokiacha, pamoja na dubu mkubwa kitandani.

"Binti yangu alizikwa akiwa hai na hoi. Maumivu ni mengi. Bado nasubiri haki."

Uchunguzi huu wa Africa Eye ulifanywa na Charlie Northcott, Helen Spooner, Maggie Andresen, Yemisi Adegoke na Ines Ward.