Ufichuzi kuhusu TB Joshua: YouTube Yaifunga chaneli ya Emmanuel TV inayomilikiwa na kanisa lake

Emmanuel TV ilikuwa na wafuasi zaidi ya nusu milioni kwenye YouTube na mamia ya mamilioni ya maoni.

Muhtasari

•YouTube imesitisha chaneli ya kanisa kuu la mwinjilisti wa televisheni wa Nigeria TB Joshua kwa kukiuka sera zake za matamshi ya chuki.

•TB Joshua alisifika kwa huduma zake za "uponyaji" na akarekodi mamia ya huduma ambazo zilidai kumuonyesha akiwaponya watu.

TB Joshua
TB Joshua
Image: HISANI

Mtandao wa YouTube umesitisha chaneli ya kanisa kuu la mwinjilisti wa televisheni wa Nigeria TB Joshua kwa kukiuka sera zake za matamshi ya chuki.

Hatua hiyo inajiri wiki kadhaa baada ya uchunguzi wa BBC na OpenDemocracy kufichua ushahidi wa kuenea kwa unyanyasaji wa kingono na mateso yaliotekelezwa na mhubiri.

Emmanuel TV ilichukua jukumu muhimu katika kuimarika kwake kutoka kuwa mchungaji wa ndani hadi kuwa nyota wa kimataifa.

TB Joshua alifariki mwaka 2021, lakini Kanisa lake la Synagogue Church of All Nations (Scoan) sasa linaongozwa na mkewe Evelyn Joshua.

Kanisa halijazungumza lolote kuhusu kuondolewa kwake, lakini limesema madai ya awali ya makosa hayo “hayakuwa na msingi”.

Emmanuel TV ilikuwa na wafuasi zaidi ya nusu milioni kwenye YouTube na mamia ya mamilioni ya maoni.

Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miaka mitatu kwa kituo chake cha YouTube kusimamishwa, kufuatia ukiukaji wa awali wa miongozo ya jumuiya ya mfumo huo.

Kama sehemu ya uchunguzi na BBC, OpenDemocracy ilichanganua uwepo wa Emmanuel TV mtandaoni, na kupata angalau video 50 za "matusi" kwenye YouTube.

Timu yao iliripoti video hizo kwa YouTube na akaunti ilisimamishwa tarehe 29 Januari.

Katika maoni kwa BBC, jukwaa la kushiriki video linalomilikiwa na Google lilisema Emmanuel TV "imesitishwa kwa kukiuka... sera za matamshi ya chuki".

TB Joshua alisifika kwa huduma zake za "uponyaji" na akarekodi mamia ya huduma ambazo zilidai kumuonyesha akiwaponya walemavu wa mwili na wagonjwa sugu - ambazo washiriki wengi wa zamani wa kanisa hilo wamezikataa.

Maudhui ya OpenDemocracy yaliyoripotiwa ni pamoja na picha za Emmanuel TV za watu walio na matatizo ya afya ya akili wakiwa wamefungwa minyororo, kesi za taarifa potofu za kimatibabu na mifano ya kampeni za kupaka matope wanawake waliozungumza kuhusu unyanyasaji wa kingono wa TB Joshua.

Chaneli ya satelaiti ya Emmanuel TV ilirushwa tarehe 17 Januari na MultiChoice, kampuni ya Afrika Kusini inayoendesha huduma za satelaiti maarufu za DStv na GOTv.

Kwa miaka mingi, chaneli hiyo ilikuwa mojawapo ya mitandao ya Kikristo yenye mafanikio zaidi ulimwenguni, ikitangaza kwa mamilioni ya watu duniani kote.

Kufuatia kuchapishwa kwa uchunguzi wa BBC kuhusu TB Joshua, wachangiaji kadhaa wamezuiliwa na akaunti za kanisa na Emmanuel TV mtandaoni.

Akaunti hizi pia ziliripotiwa kwa YouTube na openDemocracy, lakini hazijaondolewa.

YouTube na majukwaa mengine ya mitandao ya kijamii yamechunguzwa vikali katika miaka ya hivi karibuni kutokana na sera zao za usalama mtandaoni.