•Katika mahojiano ya miaka mitano iliyopita, mamake Jowie alisema alihisi uchungu ambao wazazi wa Monica walikuwa wakipitia.
•Wakati wa mahojiano, familia ya Jowie ilimtaja kuwa Mkristo na mtu anayependa Kanisa.
Miaka mitano iliyopita, familia ya Joseph Irungu almaarufu Jowie haikuwa na uhakika kuhusu hatima ya kesi ya mauaji ambayo mwana wao alikabiliwa nayo.
Kisa, walikuwa na matumaini kwamba ingebainika mtoto wao hakuwa na hatia.
Lakini mnamo Ijumaa, Mahakama Kuu ilimpata Jowie na hatia ya kumuua mfanyabiashara Monica Kimani huku aliyekuwa mchumba wake, na ambaye alikuwa mtangazaji wa TV Jackie Maribe akiachiliwa huru.
Hakimu Grace Nzioka alisema upande wa mashtaka umethibitisha bila shaka kuwa Irungu alimuua Kimani.
Katika mahojiano ya kipekee na NTV miaka mitano iliyopita, mamake Jowie alisema alihisi uchungu ambao wazazi wa Monica walikuwa wakipitia.
Aliomba msamaha kwa familia ya Monica ikiwa mwanawe angepatikana na hatia ya mauaji yake.
"Nawahurumia kama mzazi na naskia ile uchungu ya mtu kupoteza mtoto wake lakini ile kitu inanishangaza nashindwa kweli ni mtoto wangu, hilo ndilo swali najiuliza na ningependa tu Mungu afunue ukweli ndio niweze kuheal kwa sababu niko na shida," alisema.
Wakati wa mahojiano, familia ya Jowie ilimtaja kuwa Mkristo na mtu anayependa Kanisa.
Babake alifichua kuwa Jowie alikuwa mshiriki wa kwaya alipokuwa akikua.
Jowie ni mwanamuziki wa injili na ametoa nyimbo kadhaa huku wimbo wake wa hivi punde zaidi ukiwa siku ya Ijumaa ambao ulipakiwa kwenye chaneli yake ya YouTube saa chache baada ya yeye kupatikana na hatia.
Katika wimbo huo uliopewa jina la Nakuabudu, Jowie anasema anamrudia Mungu huku akilia miguuni pake.
"Mikononi mwako Yesu, narejea. Miguuni mwako Yesu, nalilia," Irungu anaimba.
Baada ya kupatikana na hatia, Jowie alitiwa rumande akisubiri kuhukumiwa kwake tarehe 8 Machi 2024.
Hata wakati Wakenya wakisubiri kuhukumiwa kwake, Jowie, kupitia wakili wake Profesa Hassan Nandwa alisema atakata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu.
Alisema ingawa wanaheshimu uamuzi huo, hawakubaliani na matokeo yake.