Kwanini baadhi ya watu wana tabia ya kupenda kula kula?

Lipi la kufanya kuepuka kula kupita kiasi? ‘Utafiti unatuambia njaa ya namna hiyo inaweza kupungua wakati wa kupunguza uzito," anajibu Dkt Mead.

Muhtasari
  • Ijapokuwa kiwango fulani cha furaha kinahusika katika ulaji wa chakula. Tabia ya kula kula mara nyingi huhusishwa na jamii ambapo chakula ni rahisi kukipata.

Je, umewahi kula vitafunio, hata baada ya kushiba, kwa ajili tu ya kujifurahisha? Ikiwa ndivyo, unaweza kuwa mwathirika wa tabia ya kula kula ambayo wataalamu wanaiita “hedonic eating.”

Wanasayansi wanaelezea tabia hii ya kula kula haichochewi na njaa, bali na hamu ya kula kwa lengo la kujifurahisha. Tabia hii ya kula inatokana na neno la Kigiriki "hedone," linalomaanisha "raha" (Hedone pia ni mungu wa furaha wa Kigiriki).

Ijapokuwa kiwango fulani cha furaha kinahusika katika ulaji wa chakula. Tabia ya kula kula mara nyingi huhusishwa na jamii ambapo chakula ni rahisi kukipata.

Mwili wetu hutumia nishati ya chakula, ambayo ni kalori tunayoipata kutokana na vyakula na vinywaji tunavyotumia. Tunapochoma kalori zaidi kuliko tunavyopokea, mwili wetu hujibu kwa kuongeza hamu ya kutaka kula.

Tumbo letu lina mfumo wa homoni ambao huuambia ubongo kuwa tumbo ni tupu. Hii inaitwa "njaa ya kimwili."

Lakini hapa tunazungumzia tabia ya kupenda kula wakati hatuhisi njaa ya kibaolojia, lakini kimsingi tunaendeshwa na hamu ya kula chakula kwa ajili ya furaha.

James Stubbs, profesa wa chakula katika Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza anasema, "kwa watu wengine, chakula ni starehe. Tabia zetu za ulaji zinahusishwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na mihemko, kuepuka mfadhaiko na usumbufu. Na tabia hiyo hufifisha tofauti kati ya njaa ya kweli na njaa ya starehe.’’

"Kwa kawaida tunaviona vyakula vyenye mafuta mengi, chumvi na sukari vinavutia kwa sababu ni vyanzo vya nishati," anaeleza Dk Bethan Mead, mhadhiri mkuu na mtafiti katika taasisi ya Appetite Research Group ya chuo kikuu cha Liverpool.

Unene wa kupindukia kwa kula vyakula vyenye mafuta mengi, chumvi na sukari pia huchukuliwa kuwa moja ya tabia ya ulaji wa mara kwa mara.

"Sasa tumezungukwa na wingi wa vyakula vitamu ambavyo ni rahisi kuvipata na viko tayari kwa kuliwa," anasema Profesa Stubbs.

"Vyakula hivyo vinachangia uzito na unene katika jamii ya kisasa. Haishangazi kwamba mtu mmoja kati ya wanane kwa sasa ni mnene kupita kiasi.”

Utafiti uliochapishwa Januari 2024 katika Jarida la Lishe ya Binadamu na Dietetics ulichambua uhusiano kati ya kupenda kula na unene.

Lipi la kufanya?

Lipi la kufanya kuepuka kula kupita kiasi? ‘Utafiti unatuambia njaa ya namna hiyo inaweza kupungua wakati wa kupunguza uzito," anajibu Dkt Mead.

‘Kupunguza uzito kwa kuanzisha tabia mpya ya kula na kufuata mtindo mpya wa maisha wenye afya sio rahisi. Lakini ni jambo linalowezekana,’’ anasema Profesa Stubbs.

Kwa mfano, ikiwa unataka kuongeza shughuli zako za kila siku, fikiria kuhusu shughuli zinazokupa furaha zaidi. Kwenda kwenye mazoezi? Kutembea na marafiki au kucheza?

“Jambo muhimu ni kujaribu kuelewa ni mambo gani yanakupa furaha katika maisha yako na kujaribu kuyapatanisha mazoea yako mapya na mambo yanayokupa raha.

Kula kwa uangalifu kunaweza pia kuwa njia ya kuzuia ulaji wa kupita kiasi.

"Hatutaki kuwazuia watu kula vyakula wapendavyo," anasema Profesa Stubbs, "tunataka kuwaelekeza ulaji bora wenye furaha."

Ikiwezekana kukuza uhusiano mzuri na chakula, bila kuathiri raha ambayo vyakula vyenye ladha nyingi hutoa.

"Ikiwa unakula 80% ya vyakula vilivyo na kalorii kidogo, virutubishi kidogo, una 20% iliyobaki kufurahia chipsi ambazo huongeza furaha maishani,’ anasema Profesa Stubbs.