Kutakana na sokwe asiyetaka kutenganishwa na mtoto wake aliyekufa miezi 3 iliyopita

Tangu kifo cha mwanawe, sokwe huyo mwenye umri wa miaka 21 hajataka kuuwacha mwili wa mtoto wake

Muhtasari

•Mwili huo umepitia mchakato wa kuoza kawaida na hifadhi hiyo imehakikisha hilo halisababishi shida za kiafya.

•Hajaonyesha matatizo ya kiafya, kutokana na kuwa na mwili wa mtoto wake aliyekufa miezi kadhaa iliyopita.

Sokwe Natalia alipoteza mtoto wake baada ya siku 14 tangu kumzaa.
Sokwe Natalia alipoteza mtoto wake baada ya siku 14 tangu kumzaa.
Image: BBC

Hii ni mara ya pili kwa sokwe Natalia kupoteza mtoto. Alijifungua mwanzoni mwa Februari mwaka jana na kila kitu kilionekana kuwa sawa katika mbuga ya wanyama ya Bioparc, katika jiji la Valencia, Uhispania.

''Lakini ghafla mtoto wake alidhoofika na akafariki. Hatujui sababu haswa ni nini, lakini tunadhani mama hakuwa akitoa maziwa ya kutosha," anasema mkurugenzi wa Bioparc, Miguel Casares.

Tangu kifo cha mwanawe, sokwe huyo mwenye umri wa miaka 21 hajataka kuuwacha mwili wa mtoto wake. Ameubeba kwa zaidi ya miezi mitatu huku akiendelea na shughuli zake za kila siku.

"Hii ni tabia ambaye hutokea kwa sokwe wa kike baada ya watoto wao wachanga kufariki kwenye mbuga za wanyama," anaelezea Casares, ambaye ni mtaalamu wa mifugo.

''Sokwe wa kike wanajuulikana kubeba watoto wao hadi miezi minne. Si mara zote hutokea, lakini jike anaweza kubeba mtoto aliyekufa kwa siku chache au wiki chache, na pia katika baadhi ya kesi kama hii, miezi michache," anasema Casares.

Katika bustani hii ya wanyama, wageni wamemwona mama sokwe akiwa na mtoto wake. Na imesababisha hisia za kila aina.

Mwili huo umepitia mchakato wa kuoza kikawaida na hifadhi hiyo imehakikisha hilo halisababishi shida za kiafya, ili kumruhusu Natalia kujitenga polepole na mwanawe hadi pale atakapokuwa tayari.

Kuundoa mwili sio chagua sahihi

Image: BBC

Sokwe huyo alipoteza mtoto mwaka 2018 na katika tukio hilo aliuacha mwili wake siku chache tu. Wakati huu hali imekuwa tofauti.

Kama ilivyo kwa sokwe wengine wanaoishi katika mazingira ya asili au yanayodhibitiwa, sokwe katika bustani ya Valencia Bioparc wanaishi katika familia, urafiki na umoja.

"Katika siku za kwanza walikuwa karibu naye sana, walikumbatiana. Kilikuwa ni kitu cha kushangaza kwa sababu kilifanana na kile kinachotokea kwa binaadamu," anaeleza Casares.

Baada ya muda, sokwe wengine - kutoka jamii zingine - waliendelea na taratibu zao za maisha ya kila siku. Lakini Natalia alichagua kutouacha mwili wa mtoto wake.

Wataalamu wa bustani walitathmini hali hiyo na kuamua kumwacha aendelee kumshikilia kwani hilo ndilo lilikuwa jambo bora kwake. Kwani kuingilia kati kuuondoa mwili - ingekuwa kazi ngumu na ya hatari.

"Familia ya sokwe huyo iko pamoja nae wakati wote, hivyo kama tungetaka kumtoa mtoto ingebidi tumdunge sindano ya usingizi mama huyo, na bila shaka tungelazimika kuwadunga sindano ya usingizi wana familia wengine kadhaa," anasema mkurugenzi wa Bioparc.

"Na kuna jike mwingine, ambaye ni dada yake, na ana mtoto mdogo, kitendo hicho kingemuweka mtoto huyo aliyehai hatarini. Tuliachana na chaguo hilo."

"Kifo pia ni sehemu ya maisha"

Image: BBC

Maelezo ya picha,Wageni wamepata hisia za huruma waliposikia mkasa wa Natalia.

Sokwe Natalia anafanya shughuli zake za kila siku. Hajaonyesha matatizo ya kiafya, kutokana na kuwa na mwili wa mtoto wake aliyekufa miezi kadhaa iliyopita.

"Tumekuwa tukifuatilia hali ya afya ya wanyama wakubwa na hatujaona matatizo yoyote. Lakini, bila shaka, mtoto ameoza. Ni mchakato wa asili. Lakini kwa bahati nzuri, sokwe wana mfumo wa kinga wenye nguvu sana," anaelezea Casares.

Ikibidi, wataalamu wa mbuga wanaweza kuingilia kati, lakini kwanza wamemuacha mama akubaliane na matokeo yeye mwenyewe kwa ajili ya ustawi wake.

Casares anasisitiza ukweli kwamba, licha ya kuwa katika mazingira yanayodhibitiwa, sokwe katika bustani hii si wanyama wa kufugwa. Hufuata mifumo sawa na ile katika mazingira mengine ya asili.

Image: BBC

"Tabia hii hutokea kwa wanyama wengine pia, sio tu kwa sokwe, hutokea kwa nyani na tembo, wanyama ambao wana akili sana na wenye uhusiano mkubwa sana kati ya mama na watoto na tabia ya kuishi kifamilia," anabainisha.

"Kwenye bustani ya wanyama, sio wanyama wakubwa na watoto kucheza pekee. Kifo pia ni sehemu ya maisha na wakati mwingine wanyama hufa."

Ingawa inashangaza na imewavutia watu wengi, haswa watoto wadogo, wamiliki wa bustani hiyo wapo hapo kutoa maelezo kwa wageni kuhusu tukio hilo.

"Walio wengi wamelielewa, wameonyesha huruma na heshima kwa mama ambaye yuko katika majonzi ya kufiwa na mtoto," anaelezea Casares.