"Usinyamaze!" Mwanadada jasiri aliyewazomea viongozi wa Uasin Gishu amgeukia Ruto kwa ujumbe mzito

Mercy sasa amemgeukia rais William Ruto akitaka aingilie kati suala la sakata ya elimu ya Finland lililopamba moto.

Muhtasari

•Mercy alimwomba rais William Ruto kuwapigania wanafunzi na wazazi walioathirika na sakata hilo huku akimthibitishia kuwa kuna tatizo kubwa katika kaunti ya Uasin Gishu.

•Msichana huyo aliweka wazi kuwa yeye na walalamishi wengine wanadai pesa ambazo walikuwa wamelipa kwa mradi huo uliofeli wa elimu ya ng'ambo.

akiwasuta hadharani viongozi wa Uasin Gishu siku ya Jumatatu.
Mercy Tarus akiwasuta hadharani viongozi wa Uasin Gishu siku ya Jumatatu.
Image: HISANI

Mercy Tarus, msichana mhitimu wa Chuo Kikuu cha Kabarak ambaye amejizolea umaarufu mkubwa  baada ya video yake akiwakashifu viongozi wa Uasin Gishu hadharani kuhusu sakata ya elimu ya Finland ilivuma kwenye mitandao ya kijamii sasa amemgeukia rais William Ruto akitaka aingilie kati suala hilo lililopamba moto.

Siku  ya  Jumatatu, Mercy alirekodiwa akimkosoa gavana wa Uasin Gishu Jonathan Bii, seneta Jackson Mandago na naibu gavana John Barorot. Wakenya wengi walimpongeza kwa ujasiri wake alipokuwa akiwahutubia viongozi watatu wakuu wa kaunti.

Wakati akizungumza na mwanahabari wa Citizen Tv siku ya  Jumatano wakati wa maandamano ya wazazi na wanafunzi katika mji wa Eldoret, Mercy alimwomba rais William Ruto kuwapigania wanafunzi na wazazi walioathirika na sakata hilo huku akimthibitishia kuwa kuna tatizo kubwa katika kaunti ya Uasin Gishu.

“Tafadhali tupiganie, Uasin Gishu inawaka. Kunawaka, tunaungua, tunaumia, tuko na msongo wa mawazo, tunahitaji pesa zetu!” Mercy alisema.

Aliongeza, “Hii serikali ilikua ya Hustler, sasa hustler ametafuta pesa yake hiyo kidogo yenye amepata. Kama mimi nauza uji. Nimeenda nimehustle nimepata pesa zangu kidogo za uji na mandazi nikuje nilipe nijaribu kutafuta maisha mazuri kwa ajili yangu alafu mtu anakuja kuchukua pesa zangu, watoto wake hawako Kenya wameenda majuu na sasa unanyamaza. Tafadhali, tafadhali rais wetu, usinyamaze. Kunaungua, tulikupigia kura, tunaomba utupiganie. Na ofisi yako tupiganie kabisa tunaumia.

Msichana huyo aliweka wazi kuwa yeye na walalamishi wengine wanadai pesa ambazo walikuwa wamelipa kwa mradi huo uliofeli wa elimu ya ng'ambo.

Alisema kwa sasa wamechoshwa na maelezo na hadithi nyingi zinazotolewa na viongozi wa kaunti kila wanapoulizwa kuhusu kilichotokea.

“Nimesikia stori tangu nilipe pesa zangu kwanza na nimechoshwa na hadithi hizo. Nimechoka sana na hadithi. Hatukumuweka hapo ndio akuje atupatie stori, stori tunaweza pata mitandaoni. Tumechoka tunataka pesa yetu,” alisema.

Mercy Tarus amekuwa akivuma kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kwa siku mbili zilizopita huku wanamitandao Wakenya wakiendelea kumsifu kwa ujasiri mkubwa  ambao alionyesha wakati alipokuwa akikabiliana hadharani na gavana Bii, Mandago na Barorot katika mkutano uliofanyika Jumatatu.