Raila alinipa tagi ya 'Watermelon' na ninaipenda, Kalonzo asema

Muhtasari
  • Akizungumza nyumbani kwake Tseikuru, Kalonzo alisema tikiti maji ni tunda zuri na watu wanapaswa kuacha kulifanyia mzaha
HE Kalonzo Musyoka akihutubia wanahabari katika Kituo cha Amri, Karen mnamo Jumanne Machi 1 wakati wa mkutano na wanahabari kuhusu mikataba ya NASA kati ya Raila Odinga na Kalonzo wakati wa uchaguzi wa 2017.
Image: Wilfred Nyangaresi

Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amesema ni Raila aliyempa tagi ya Tikiti maji.

Akizungumza nyumbani kwake Tseikuru, Kalonzo alisema tikiti maji ni tunda zuri na watu wanapaswa kuacha kulifanyia mzaha.

“Ni Raila ndiye aliyenipa tagi hiyo. Yeye ni kaka yangu, kwa hivyo hakuna shida,” Kalonzo alisema kwenye mahojiano na KTN.

Kalonzo alisema kuwa hii itakuwa mara ya tatu akimuunga mkono Raila Odinga kama mgombeaji urais.

"Ikiwa watu wataniuliza nimuunge mkono Raila Odinga mara 20, nitamuunga mkono ikiwa ndivyo itamaanisha kuweka taifa hili pamoja," alisema.

Alipoulizwa iwapo anadhani mkataba huo uliotiwa saini siku ya Jumamosi utatekelezwa, Kalonzo amesema kuwa itategemea nia njema ya Raila Odinga.

“Naomba awe rais ajaye. Nitazunguka nikiwaambia Wakenya wamfanyie kampeni Raila,” akaongeza.

Mwaka jana Kalonzo alisema hatamuunga mkono Raila katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Katika mahojiano na NTV, Kalonzo alisema amefedheheshwa chini ya muungano wa NASA na hangefikiria kuungana na Raila kwa mara ya tatu.

 Jumamosi, wakati wa mkutano wa Azimio la Umoja, mkuu wa chama cha Wiper alisema ataunga mkono azma ya Raila kwa mara ya tatu.

"Nilidhani Raila ataniidhinisha urais wakati huu lakini kwa moyo mwema, nitamuunga mkono. Raila Tosha," Kalonzo alisema.