DCI yafichua uchunguzi mpya dhidi ya kifo cha mwanafunzi aliyefariki kwenye bweni la Gatanga CMM miaka 3 iliyopita

Muhtasari

• DCI yakamilisha uchunguzi dhidi ya mauaji ya kikatili ya mwanafunzi Ebby Noelle Samuel aliyepatikana amefariki katika bweni kwa njia za kutatanisha.

• Awali ripoti ya upasuaji wa mwili wa Ebby ilikuwa imeonesha kwamba mwanafunzi huyo alifariki kutokana na kugongwa na kifaa Kizito kichwani.

Ebby Noelle Samuel, mwanafunzi wa Gatanga CCM aliyefariki kwa njia ya kutatanisha
Ebby Noelle Samuel, mwanafunzi wa Gatanga CCM aliyefariki kwa njia ya kutatanisha
Image: HISANI

Idara ya ujasusis DCI imetoa taarifa kwamba hatimaye wamekaribia kutamatisha uchunguzi dhidi ya kifo cha kutatanisha cha mwanafunzi wa shule ya upili ya Gatanga CMM aliyepatikana amefariki katika bwenu la shule hilo mwezi Machi mwaka wa 2019.

Katika kile ambacho DCI walidokeza kwamba ni mchezo uliokuwa unachezwa na wakuu wa shule hiyo ili kuficha ukweli wa kilichosababisha kifo cha msichana huyo kwa jina Ebby Samwel, iliwabidi majasusi hao kufuata wanafunzi mashahidi hadi nyumbani kwani wakati wa likizo ili kurekodi taarifa baada ya kugundulika kwamba wanafunzi hao walikuwa wanatishiwa shuleni dhidi ya kutoa Ushahidi wao.

Ebby ambaye alikuwa kidato cha kwanza wakati huo alipatikana amefariki katika hali ya ukakasi ambapo uongozi wa shule ulisema kwamba alidondoka kutoka kitandani na kuanguka sakafuni kupelekea kifo chake.

Baada ya taarifa hiyo ya uongozi wa shule kuonekana kukinzana na taarifa iliyoandikishwa na wanafunzi, DCI iliamua kulivalia njuga suala hilo kwa undani zaidi ili kubaini ukweli na familia ya Ebby kuujua ukweli wa kifo cha mwanao.

Waligundua kwamba uongozi wa shule ulikuwa unatishia wanafunzi waliokuwa tayari kutoa Ushahidi wao na hivyo wakachukua mkondo tofauti wa kuwafuata wanafunzi mashahidi hadi nyumbani wakati wa likizo ambapo sasa wamedokeza kwamba uchunguzi tayari umeshakamilika na hivi karibuni watuhumiwa watachukuliwa hatua za kisheria.

“Timu ya majasusi wetu imebaini kuwa katika usiku huo wa maafa, Ebby alishambuliwa vikali na mmoja kati ya wasimamizi wakuu wa shule kwa madai kuwa nywele zake zilikuwa zimepambwa kinyume na kanuni za shule. Hii ilitokea wakati wa maandalizi ya jioni, dakika chache kabla ya kengele ya saa tatu usiku kugongwa. Ebby aliingia kulala usiku huo akiwa na majeraha mabaya. Hiyo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho kwa marafiki wa Ebby kumuona akiwa hai, kwani jitihada zao za kumwamsha asubuhi iliyofuata ziliambulia patupu,” DCI walieleza kupitia facebook yao.

Awali ripoti ya upasuaji wa mwili wa Ebby ilikuwa imeonesha kwamba mwanafunzi huyo alifariki kutokana na kugongwa na kifaa Kizito kichwani.