Jamaa adaiwa kutilia mashemeji sumu kwa chakula

Baada ya mama na watoto wake kula chakula hicho walianza kulalamikia maumivu tumboni.

Muhtasari

• Mama na watoto wake wanne walilazwa hospitalini ya Lugari, kaunti ya Kakamega baada yao kula chakula kinachodaiwa kuwekwa sumu na mpenzi wa bintiye mmoja.

• Walianza kufanya juhudi  zao za kutafuta usaidizi kutoka kwa majirani ila hakuna aliyewasikia.

Mama na watoto walazwa baada ya kula Githeri iliyotiwa sumu na mpenzi wa binti wa familia
BBC Mama na watoto walazwa baada ya kula Githeri iliyotiwa sumu na mpenzi wa binti wa familia
Image: BBC

Siku ya Jumapili, Oktoba 2, Mama na watoto wake wanne walilazwa hospitalini ya Lugari, kaunti ya Kakamega baada yao kula chakula kinachodaiwa kuwekwa sumu na mpenzi wa bintiye mmoja.

Evelyne Ongachi, Mama wa watoto hao,  alichemsha Githeri na kukiacha jikoni kikichemka na baadae kuhudhuria ibada ya kanisa. Waliporudi nyumbani, mmoja wa wanafamilia alifika jikoni kukaanga chakula hicho na kuwapakulia wengine.

Masaa machache baadaye, familia nzima ilianza kulalamiika kuhusu  maumivu ya tumbo kisha wakaanza kutapika.

"Kila mara, mimi huweka chakula cha watoto jikoni. Sasa niliporudi nikaambiwa watoto wamebakisha chakula. Watoto walikaanga githeri kilichobaki na kutupakulia. Mara tu tulipomaliza kula, shida ikaanza,” mama alisimulia.

Walianza kufanya juhudi  zao za kutafuta usaidizi kutoka kwa majirani ila hakuna aliyewasikia.

Walilazimika kuvumilia maumivu hayo usiku kucha hadi asubuhi walipopata usaidizi na kukimbizwa hospitalini.

“Asubuhi ya Jumatatu, jirani yangu, ambaye huwa tunaenda naye kazini, alikuja kunichukua ili tuende kazini. Yeye ndiye aliyetusaidia kwa sababu alifanya mipango ya haraka na kutukimbiza hospitalini,” Everlyne alieleza kituo kimoja cha habari humu nchini.

Mama huyo alisema anashuku mpenzi wa bintiye ndiye anayehusika katika kitendo hicho cha kusikitisha.

Alisema mpenzi wa bintiye na ambaye pia ni jirani yao, ni mwenye vurugu akitoa mfano wa siku chache zilizopita ambapo alifika nyumbani kwao na kuzua zogo kabla ya  majirani kumzuia.

"Mpenzi wangu amezaa mtoto na mvulana jarini. Juzi kijana huyo alikuja na kusababisha tafrani nyumbani kwangu na kusema ikiwa si kuua mtu atafanya jambo ambalo lazima litangazwe kwenye vyombo vya habari,” mamake binti alilalamika.