Nilihudumu vyema chini ya utawala wa Uhuru hadi aliponitupa nje-Kindiki

Alisema atafurahi kufanya kazi chini ya Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua pamoja na maafisa wengine wa serikali.

Muhtasari
  • Akizungumza Jumanne alipofika mbele ya Kamati ya Bunge ya Kitaifa kuhusu uteuzi wa kuhakikiwa, Kindiki alisisitiza kuwa alitupwa nje bila sababu
KITHURE KINDIKI AKIWA MBELE YA KAMATI YA USAILI YA BUNGE LA KITAIFA
Image: EZEKIEL AMINGA

Aliyekuwa Mbunge wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki amesema alihudumu vyema chini ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta hadi alipofukuzwa.

Akizungumza Jumanne alipofika mbele ya Kamati ya Bunge ya Kitaifa kuhusu uteuzi wa kuhakikiwa, Kindiki alisisitiza kuwa alitupwa nje bila sababu.

"Uhuru Kenyatta ndiye Rais wa zamani wa Kenya. Pia nilihudumu chini yake vizuri sana hadi akanitupa nje bila sababu," alisema.

Seneta huyo wa zamani alikuwa amejitokeza kupigwa msasa  kufuatia kuteuliwa kwake na Rais William Ruto kuhudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa.

Alisema atafurahi kufanya kazi chini ya Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua pamoja na maafisa wengine wa serikali.

Kithure alishtakiwa miongoni mwa mambo mengine, kula njama na Kipchumba Murkomen ambaye pia alikuwa amefukuzwa kama kiongozi wa wengi ili kutupilia mbali hati ya Uhuru ya kuhamisha majukumu ya serikali ya Kaunti ya Nairobi hadi serikali ya kitaifa.

Wafuasi wa Uhuru pia walimshutumu Kithure kwa kuwahamasisha maseneta wa Jubilee dhidi ya kile walichokitaja kuwa ‘matakwa ya chama’.

Kindiki alieleza kuwa vyanzo vyake vya utajiri vilijumuisha taaluma yake ya sheria, mshahara wa kazi yake ya awali pamoja na ujasiriamali.

“Kwa sasa mimi ni wakili katika Mahakama Kuu ambako ninafanya kazi ya uanasheria.

"Mimi pia ni mfanyabiashara ninayefanya biashara kadhaa, SME na pia ni mshauri wa mashirika ya ndani na kimataifa," Kindiki aliiambia kamati.