Serikali ya Mahasla: Fahamu utajiri wa mawaziri wateule katika serikali ya Ruto

Katika kuimarisha utendakazi wake, rais Ruto alitoa orodha ya baraza lake la mawaziri ambao sharti wapitie mchakato wa kuhojiwa bungeni kabla ya kuidhinishwa.

Muhtasari

• Mawaziri hao ambao wengi wana uzoefu mkubwa katika siasa waliteuliwa takribani mwezi mmoja uliopita na rais Ruto.

baraza la mawaziri
baraza la mawaziri
Image: maktaba

Jumatatu bunge la kitaifa liliwahoji baadhi ya mawaziri wataule watakaohudumu katika baraza la mawaziri la serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na rais William Ruto.

Katika serikali hiyo ambayo wengi wanaichukulia kama ya watu wapambanaji wenye uchumi wa kadri almaarufu Hustlers, mawaziri hao wateule walishangaza wengi baada ya kufichua utajiri wao ambao ni wa mamilioni ya pesa.

Katika orodha hii, tunakuandalia orodha ya utajiri wa baadhi ya mawaziri wale ambao walihojiwa katika bunge la kitaifa.

Musalia Mudavadi

Aliyekuwa kinara wa chama cha ANC kabla ya kuweka wazi kwamba aliachia madaraka hayo. Aliteuliwa na rais William Ruto kama mkuu wa mawaziri ambaye afisi zake zitakuwa katika majengo ya shirika la reli la Kenya.

Mudavadi alifichua kwamba utajiri wake ni wa thamani ya bilioni 4 pesa za benki kuu ya Kenya.

Aden Duale

Mbunge mara nne wa Garissa Township ambaye aliteuliwa na rais Ruto kama waziri wa ulinzi. Duale aliweka wazi mbele ya kamati ya bunge kuwa utajiri wake ni wa kima cha milioni 851, ambao wengi unatokana na biashara za nyumba za kukodisha pamoja pia na ufugaji wa ngamia.

Justine Muturi

Muturi alikuwa kama spika wa bunge la kitaifa katika bunge la awamu ya 12. Aliteuliwa kama mwanasheria mkuu wa serikali na rais Ruto. Utajiri wake ni wa thamani ya milioni 700.

Alfred Mutua

Aliyekuwa gavana wa kwanza wa Machakos kwa miaka 10 kabla ya kipindi chake rasmi kukamilika. Kiongozi huyo wa chama cha Maendeleo Chap Chap. Rais Ruto alimteua kama waziri vwa mambo ya nje na alifunguka kuwa utajiri wake ni wa thamani ya milioni 420.

Alice Wahome

Mbunge mara mbili wa Kandara. Wahome aliteuliwa na Ruto kama waziri wa maji na unyunyiziaji mimea. Akihojiwa na kamati ya bunge, aliweka wazi kwamba utajiri wake ni wa thmani ya milioni 218.

Kithure Kindiki

Kithure Kindiki ni mwanasiasa na wakili ambaye sasa ameteuliwa kwenye Baraza la Mawaziri katika serikali ya Rais William Ruto kama Waziri anayesimamia Mambo ya Ndani na Utawala wa Serikali ya Kitaifa. Alichaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2013 kuwakilisha Kaunti ya Tharaka-Nithi katika Seneti ya Kenya

Kindiki aliweka wazi kuwa thamani yake ni ksh 544m inayojumuisha ardhi na majengo, amana za benki, uwekezaji wa hisa na amana katika saccos 5 tofauti.

Aisha Jumwa

Aliyekuwa mbunge wa Malindi ambaye baada ya kushindwa kutetea kiti hicho, aliteuliwa na rais William Ruto kama waziri katika Wizara ya Utumishi wa Umma na Jinsia. Utajiri wake ni wa thamani ya milioni 100.

Prof Njuguna Ndung'u

Msomi huyu alikuwa gavana wa awali wa benki kuu ya Kenya kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na Patrick Njoroge.

Ndung'u aliteuliwa na rais Ruto kama waziri wa fedha kuchukua nafasi ya waziri anayeondoka Ukur Yattani. Thamani yake ni ya milioni 950.

Davis Chirchir

Aliteuliwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kama waziri wa Nishati na Petroli mwaka 2013. Tarehe 27 Septemba 2022, aliteuliwa tena na Rais mpya William Ruto kama waziri atayesimamia wizara ya kawi.

Akiwa mbele ya kamati ya bunge ambayo iliongozwa na spika, aliweka wazi kwamba utajiri wake ni wa thamani ya milioni 482.  Alisema utajiri wake ni kutokana na nyumba za kupangisha, kuwekeza katika ukulima wa majani chai miongoni mwa mitaji mingine.

Moses Kuria

Alikuwa mbunge wa Gatundu Kusini katika bunge la 12. Rais Ruto alimteua kama waziri wa biashara, viwanda na uwekezaji kwa vijana na alipofika mbele ya kamati ya bunge, alisema thamani yake ni ya milioni 750.

"Thamani yangu inajumuisha maendeleo ya mali isiyohamishika na hisa zinazofanyika katika biashara mbalimbali katika sekta ya viwanda, Fintech na nishati," Kuria alielezea chanzo cha utajiri wake.

Kipchumba Murkomen

Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Elgeyo Marakwet. Wakili huyo aliteuliwa kama waziri wa barabara na miundombinu. Utajiri wake ni wa thamani ya milioni 550.

Roselynda Soipan Tuya

Waziri mteule katika  wizara ya Mazingira na Misitu. Kabla ya kuteuliwa kwenye wadhfa huo, Tuya alikuwa mwakilishi wa kike katika kaunti ya Narok. Anaingia kwenye rekodi kuwa mwanamke wa kwanza kuwahi kutokea katika jamii ya Wamaasai kuhudumu kama waziri. Ana thamani ya milioni 156.

Susan Wafula Nakhumicha

Waziri mteule katika wizara ya afya ambaye anatarajiwa kuchukua nafasi ya waziri Mutahi Kagwe. Kisiasa, aliwania bila mafanikio kiti cha Uwakilishi wa Wanawake wa Trans-Nzoia mnamo 2022 baada ya kuwa mwanachama wa chama cha Ford ambapo pia ni makamu mwenyekiti wa wanawake, vijana na watoto.

Utajiri wake ni wa thamani ya milioni 101.

Zacharia Mwangi Njeru

Aliteuliwa na rais Ruto kama waziri mteule wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Miji

Utajiri wake ni wa thamani ya Shilingi milioni 80.

Peninah Malonza

Waziri mteule wa Utalii, Wanyamapori na Urithi Peninah Malonza alifika mbele ya kamati ya wabunge kwa ajili ya kuhakikiwa mnamo Jumatano alasiri. aliweka wazi utajiri wake ni wa kima cha milioni 300.