'Tupatieni miezi michache kila kitu kitakuwa sawa'' Gachagua asema kuhusu bei ya bidhaa

Bei ya bidhaa za kimsingi kama vile bei ya unga,mafuta ya kupika na gesi ya kupikia imeanza kushuka.

Muhtasari

•Rigathi aliwataka Wakenya kuipatia serikali miezi michache zaidi kufanya mageuzi ya  uchumi nchini.

•"Tuliahidi kupunguza gharama ya maisha na tayari mmeanza kuona bei ya unga na gesi ya kupikia ikishuka," alisema.

Naibu Rais William Ruto
Image: TWITTER// RIGATHI GACHAGUA

Naibu Rais Rigathi Gachagua aliwapa wakenya matumaini kuwa gharama ya maisha itashuka hivi karibuni na uchumi  utaboreshwa.

Akizungumza wakati wa ibada ya Kanisa huko Kenol, kaunti ya Murang'a mnamo Jumapili, Gachagua alisema kuwa bei ya bidhaa muhimu imeanza kushuka kutokana na juhudi zake na Rais William Ruto.

Bei ya bidhaa za kimsingi kama vile  bei ya unga,mafuta ya kupika na gesi  ya kupikia imeanza  kushuka, jambo ambalo Naibu rais anasema inaashiria kuna matumini kwa serikali yao kuboresha uchumi.

Hata hivyo, aliwataka Wakenya kuipatia serikali miezi michache zaidi kufanya mageuzi ya  uchumi nchini.

"Tuliahidi kupunguza gharama ya maisha na tayari mmeanza kuona bei ya unga na gesi ya kupikia ikishuka," alisema.

“Rais wetu hakutaka kutoa ruzuku ya unga ili kuwafurahisha kwa siku chache, tunataka kutafuta suluhu ya kudumu na hili linaweza kufanyika tu kwa kufanya mbolea iwe ya bei nafuu na ya kupatikana kwa wakulima, tupatieni miezi michache kila kitu kitakuwa sawa. ," aliongeza.

Matamshi ya Gachagua yanajiri wiki kadhaa baada ya Rais William Ruto kusema mwaka mmoja utatosha kwake kuhakikisha ameboresha uchumi wa kenya ambao umekuwa ukisambaratika katika miaka ya hivi majuzi.

Haya yanajiri huku kukiwa na wasiwasi na vilio kutoka kwa Wakenya kuhusu kupanda kwa gharama ya juu ya maisha. Mafuta na unga wa mahindi ni miongoni mwa bidhaa za kawaida ambazo bei yake imewaacha wakenya wakilalama.