Sakaja amtuza mkaazi wa Ruai aliyerekodi 'supermarket' moja ikimwaga takataka

Hili linakuja siku moja tu baada ya gavana huyo kuahidi kuwazawadi wanaorekodi na kuripoti visa vya utupaji taka haramu.

Muhtasari

• “Nina uhakika duka hili la jumla halitoweza tena kurundika takataka hovyo. Ahsante sana kwa mkaazi wa Ruai aliyerekodi na kutujuza" - Sakaja aliandika.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja amemtuza mkazi mmoja aliyerekodi na kuripoti utupaji haramu wa taka katika mtaa wa Ruai, kitongoji cha jiji.

Mwanasiasa huyo kijana alithibitisha msimamo huo katika chapisho la mtandao wa kijamii ambapo pia alipakia picha za uchafu huo.

Zawadi hiyo inajiri siku chache baada ya gavana kwa mara ya kwanza kuahidi kuwatoza faini watu waliorekodiwa kutupa taka. Aidha aliahidi kuwazawadia wale waliohusika kuangazia uovu huo kupitia polisi jamii.

“Nina uhakika duka hili la jumla halitoweza tena kurundika takataka hovyo. Ahsante sana kwa mkaazi wa Ruai aliyerekodi na kutujuza kuhusu kitendo hiki cha utupaji taka harama. Angalia M-Pesa yako,” Sakaja alidhibitisha kumzawidi mkaazi huyo.

Sakaja ana nia ya kutekeleza manifesto yake ya ‘Let’s Make Nairobi Work’ ambayo inajumuisha mipango ya kusafisha jiji.

Kampeni hiyo ilianza siku chache baada ya kuapishwa alipozuru jiji pamoja na naibu wake James Muchiri na kuwahakikishia wakazi kuwa atakabiliana na tishio la uchafu kote jijini.

Sakaja, Seneta wa zamani wa Nairobi, pia ameahidi kutekeleza utunzaji wa taka za kielektroniki, utupaji taka, na kushughulikia kwa haraka ufisadi na mgongano wa kimaslahi katika sekta ya usimamizi wa taka.

Hii, anasema, ni pamoja na mabomba ya maji na majitaka pamoja na kushughulikia usambazaji wa maji katika maeneo ambayo hayatumiki.

Wakazi wa Nairobi wameendelea kuelezea wasiwasi wao kuhusu usafi wa jiji hilo, haswa na takataka za viungani mwa jiji na katikati ya jiji (CBD).