Hatukupiga marufuku krusedi-Gavana Anyang Nyong'o afafanua

“Leo, tukiwa na meneja wa jiji, Abala Wanga, tulifanya mazungumzo na uongozi wa Makasisi kutoka eneo la Nyanza

Muhtasari
  • Harrison Mumia, rais wa Wasioamini Mungu katika Kenya aliunga mkono kupiga marufuku huduma za kidini za umma
Magavana James Ongwae (Kisii), Anyang' Nyong'o (Kisumu) na Abdi Mohamud (Wajir) wakihutubia wanahabari nje ya afisi za Baraza la Magavana huko Oracle, Westlands, Aprili 1. Picha: MAKTABA
Magavana James Ongwae (Kisii), Anyang' Nyong'o (Kisumu) na Abdi Mohamud (Wajir) wakihutubia wanahabari nje ya afisi za Baraza la Magavana huko Oracle, Westlands, Aprili 1. Picha: MAKTABA
Image: MAKTABA

Gavana wa Kisumu, Anyang' Nyong'o, mnamo Jumanne, Novemba 8, alifanya mkutano na makasisi ambapo alifafanua ripoti zinazodai kuwa alipiga marufuku mikutano ya kidini yaani krusedi.

Nyongo’ alisema kuwa kinyume na taarifa, uamuzi wake huo ulitokana na kupunguza kero za wananchi badala ya kupiga marufuku mikutano ya kidini.

“Leo, tukiwa na meneja wa jiji, Abala Wanga, tulifanya mazungumzo na uongozi wa Makasisi kutoka eneo la Nyanza wakiongozwa na Mtume Dkt Washington Ogonyo Ngede.

Kama kaunti, hatukupiga marufuku mikutano ya kidini (krusedi)bali tulitaka kudhibitiwa na kuendeshwa bila kuingilia haki za watu wengine,” alieleza.

Harrison Mumia, rais wa Wasioamini Mungu katika Kenya aliunga mkono kupiga marufuku huduma za kidini za umma.

Mumia alidai kuwa kelele zinazotolewa kutoka kwa taasisi za kidini ni mojawapo ya sababu kuu za uchafuzi wa kelele nchini Kenya.

"Hakuna mtu, bila kujali dini au madhumuni, anaweza kudai haki ya kuunda kelele hata katika majengo yake ambayo yanaweza kusafiri nje ya eneo lake na kusababisha kero kwa majirani au wengine," Mumia alisema.

Wasioamini Mungu pia walitaka serikali ya kaunti kupiga marufuku wito wa maombi ya Waislamu.