Gavana Wamatangi atoa onyo kwa wasanidi baada ya jumba kuporomoka Ruaka

Haya yanajiri saa chache baada ya takriban watu watatu kufariki na wengine kadhaa kuokolewa kutoka kwa jengo lililoporomoka eneo la Kasarani.

Muhtasari
  • Wamatangi alisema watakaopatikana wakijenga majengo kinyume cha sheria watasimamishwa, majengo yao kubomolewa na kushtakiwa mahakamani
GAVANA WA KIAMBU KIMANI WAMATANGI
Image: ANDREW KASUKU

Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi ametoa onyo kali kwa wale wanaojenga majengo kinyume cha sheria.

Wamatangi alisema watakaopatikana wakijenga majengo kinyume cha sheria watasimamishwa, majengo yao kubomolewa na kushtakiwa mahakamani.

Gavana huyo alizungumza huko Ruaka ambapo jengo la ghorofa tano lililokuwa likijengwa liliporomoka karibu na Klabu ya Fortune Alhamisi asubuhi.

"Njia ya kumaliza hii shida ni kuhakikisha kwamba haifanyiki, ata haianzi. Ndipo tukifika mahali ambapo tunaona mtu amekosa kufuata sheria, hio nyumba inasimamishwa na kubomolewa na mtu kufikishwa kortini,"Alizungumza Wamatangi siku ya Alhamisi.

Haya yanajiri saa chache baada ya takriban watu watatu kufariki na wengine kadhaa kuokolewa kutoka kwa jengo lililoporomoka eneo la Kasarani.

Wamatangi alisema tatizo hilo lazima litatuliwe haraka iwezekanavyo.

"Hatuezi kua tunangojea manyumba kama haya yaporomeke alafu watu wafe ndo tuanze utaratibu. Unakaa ni kama ni kawaida kwamba tunasema tunaenda kwa nani kufanya upelelezi."

Gavana huyo amesema kwamba tayari uchunguzi umeanza kufanyika kubaini chanzo cha jumba hilo kuporomoka.