Kivumbi kinatarajiwa bungeni jopo la JLAC likipendekeza Cherera na wenzake kutemwa

Muhtasari

• Ripoti hiyo inatarajiwa kuwasilishwa bungeni Alhamisi alasiri ili kujadiliwa.

• Ikiwa itapitishwa, basi rasi Ruto ana mamlaka ya kuwasimamisha kazi makamishna hao wanne kuanzia Ijumaa.

wakati wa mkutano uliopita na wanahabari katika hoteli ya Serena.
Makamishna wa IEBC Justus Nyangaya, makamu mwenyekiti Juliana Cherera, Irene Masit na Francis Wanderi wakati wa mkutano uliopita na wanahabari katika hoteli ya Serena.
Image: REUTERS

Kamati ya Bunge ya Haki na Masuala ya Kisheria imependekeza kuundwa kwa kamati ya kuwasikiliza Makamishna wanne wa IEBC wanaochunguzwa.

Kulingana na kamati ya bunge makamishna hao wanatuhumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa katiba, uzembe na utovu wa nidhamu wakati wa uchaguzi wa Agosti 9.

Kamati hiyo chini ya uwenyekiti wa George Murugara pia ilipendekeza Rais William Ruto kuwasimamisha kazi makamishna hao wanne wakisubiri kufikishwa mbele ya kamati maalum ya kuwachunguza.

Wanne hao ni Naibu Mwenyekiti Juliana Cherera, Justus Nyang’aya, Francis Wanderi na Irine Masit. Walitofautiana na mwenyekiti wao Wafula Chebukati kuhusu matokeo ya kura za urais na kukataa matokeo ya mwisho.

"Kamati inapendekeza kwamba Rais awasimamishe kazi kwa muda makamishna wanne kusubiri uamuzi wa kamati ya uchunguzi," alisema Murugara.

Mwenyekiti huyo wa JLAC aliwasilisha ripoti hiyo siku ya Alhamisi asubuhi. Bunge linatarajiwa kujadili ripoti hiyo Alhamisi alasiri ili kupitishwa jinsi ilivyo, kufanyia marekebisho au kuikatalia mbali.

Iwapo itapitishwa, basi Rais Ruto anaweza kuwasimamisha kazi kwa muda wanne hao Ijumaa.

Cherera na wenzake wanazidi kukumbwa na tufani kali baada ya kujitenga kutokana na matokeo ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9 kwa kile walimshutumumu mwenyekiti Wafula Chebukati kwa kuvuruga kura za urais na kumpa rais Ruto ushindi.

Mapema wiki jana, kinara wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga alikuwa amemsuta Ruto kwa kuanzisha mchakato wa kuwatimua akisema kuwa rais anafanya hivyo kulipa kisasi hata baada ya mahakama ya upeo kudumisha ushindi wake.

Odinga na Ruto walitupiana cheche za maneno kwenye Twitter huku Ruto akimshtumu Odinga kwa kuwatetea wanne hao ambao kujitenga kwao na matokeo ya IEBC nusra kulitumbukize taifa katika machafuko ya baada ya uchaguzi.

Odinga alikuwa amewataka wafuasi wa mrengo wa upinzani kukongamana katika uwanja wa Kamkunji Nairobi siku ya Jumatano wiki hii ili kuanzisha mchakato wa maandamano kuwatetea Cherera na wenzake lakini walilazimika kusitisha mkutano huo ili kutovuruga mitihani ya kitaifa inayoendelea nchini.