Matokeo ya KCPE kutangazwa wiki kesho - Waziri Machogu

Waziri huyo alisema haya wakati wa hafla ya mazishi eneo bunge la Nyaribari Masaba.

Muhtasari

• Mtihani wa KCPE ulikamilika takribani wiki mbili zilizopita huku ile ya sekondari ikitarajiwa kukamilika wiki kesho pia.

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu.
Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu.
Image: Facebook

Waziri wa elimu Ezekiel Machogu ametangaza wazi kuwa matokeo ya mitihani ya darasa la nane KCPE yatatangazwa wiki kesho.

Machogu alisema kuwa wizara yake imeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa hakuna visa vya wizi wa mitihani ya kitaifa ya sekondari KCSE ambayo inaendela kote nchini.

Machogu alikuwa akiyazungumza haya wakati wa hafla moja ya mazishi eneo bunge la Nyaribari Masaba ambapo alikuwa mbunge kabla ya kuwania ugavana wa kaunti ya Kisii katika uchaguzi uliopita wa Agosti 9.

“Wiki ijayo tunatangaza matokeo ya mtihani wa KCPE na hutasikiliza kesi zozote za udanganyifu chini ya uongozi wa Machogu. Upangaji wa alama za Cheti cha Elimu ya Sekondari cha Kenya (KCSE) unaendelea vyema na ninakuhakikishia, matokeo hayatakuwa na dosari zozote,” alisema waziri Machogu.

Mitihani ya KCPE ilikamilika mwanzoni mwa mwezi wa Desemba ambapo ni takribani wiki moja na siku kadhaa.

Matokeo hayo yatatoka siku chache tu kuelekea sherehe za Krismas, wakati ambapo mitihani ya kidato cha nne itakuwa inakamilika pia kote nchini.

KCSE iling’oa nanga mwanzoni mwa mwezi hu wa Desemba kwa wiki tatu hadi tarehe 23 Desemba.

Haya yatakuwa matokeo ya kwanza kutangazwa na waziri huyo mpya ambaye aliteuliwa na kupitishwa na bunge kuhudumu katika baraza la mawaziri wa rais Ruto kama waziri wa elimu, wizara ambayo ilikuwa imeshikiliwa kwa  muda mrefu na waziri profesa George Magoha.