Waziri Kindiki aapa kukabiliana na biashara ya pombe haramu

Hatuna uhakika wa siku zijazo. Vile vile tutakavyokabiliana na majambazi ndivyo tutakavyopambana na pombe haramu."

Muhtasari
  • Waziri Kindiki aliwahakikishia viongozi waliohudhuria kwamba hataacha lolote katika kuhakikisha kuwa usalama umeimarishwa katika eneo hilo
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI KITHURE KINDIKI
Image: KWA HISANI

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki ameapa kuzidisha vita dhidi ya visa vinavyokithiri vya utumizi wa dawa za kulevya na ukosefu wa usalama katika Kaunti ya Kiambu.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua kitengo cha Cianda huko Kiambaa Jumatano, Waziri Kindiki aliwahakikishia viongozi waliohudhuria kwamba hataacha lolote katika kuhakikisha kuwa usalama umeimarishwa katika eneo hilo.

Aliwakemea wanaojihusisha na utengenezaji wa pombe haramu na kusambaza pombe haramu katika eneo hilo huku akionya kuwa hatakubali vitendo haramu vinavyofanywa mkoani humo kwa kugharimu vizazi vijavyo.

"Kuna vitishio vitatu vya  kiusalama; ugaidi, ujambazi na pombe haramu, dawa za kulevya na utumiaji wa dawa za kulevya. Hizo ni matishio makubwa kwa usalama wa taifa letu," alisema.

"Isipokuwa tunafanya jambo na tukalifanya haraka tunakabiliwa na mgogoro wa vizazi. Hatuna uhakika wa siku zijazo. Vile vile tutakavyokabiliana na majambazi ndivyo tutakavyopambana na pombe haramu."