Huwezi kuunganisha taifa kwa kununua wabunge wa upinzani,Maanzo kwa Ruto

Akizungumza Jumatatu, Seneta huyo alisema kuwa Rais William Ruto hawezi kuunganisha nchi kwa 'kununua' upinzani.

Muhtasari
  • Ruto amesema hadharani serikali yake iko tayari kufanya kazi na yeyote licha ya mgawanyiko wa kisiasa

Seneta wa Makueni Dan Maanzo amejadili mjadala unaoendelea kuhusu  wabunge wa Azimio wanaofanya kazi na serikali ya Kenya Kwanza, na waliokutana na Rais Ruto IKulu wiki jana.

Akizungumza Jumatatu, Seneta huyo alisema kuwa Rais William Ruto hawezi kuunganisha nchi kwa 'kununua' upinzani.

"Moja ya majukumu makubwa ya Rais ni kuhakikisha anakuwa na taifa lenye amani na umoja. Hilo haliwezi kutokea kwa kuwanunua wabunge ili kupata wengi," Maanzo alisema.

Rais Ruto amekashifu wakosoaji kuhusu uamuzi wake wa kukutana na viongozi nje ya serikali.

Ruto amesema hadharani serikali yake iko tayari kufanya kazi na yeyote licha ya mgawanyiko wa kisiasa.

Tayari amekutana na baadhi ya wabunge wa Nyanza na viongozi wa Jubilee kutoka muungano wa Azimio la Umoja.

Hatua hiyo inaonekana kuwa mojawapo ya mikakati ya Rais kukabiliana na kinara wa upinzani Raila Odinga ambaye anafanya mikutano ya 'kupinga Ruto'.

Mwishoni mwa juma, viongozi wa ODM walitoa wito wa kufukuzwa kwa viongozi hao waliokutana na Ruto.