Cherargei:Wanachama wa Azimio wanapaswa kuondolewa Serikalini

Seneta huyo wa Nandi aliendelea kudai kuwa hakuna maana kuwa na watumishi wa umma wanaofanya kazi chini ya rais wanayempinga

Muhtasari
  • "Katika serikali hii, bado kuna mabaki mengi wa Azimio One Kenya Alliance katika nyadhifa za juu na wanapaswa kuonyeshwa mlango
Seneta wa Nandi, Samson Cherargei
Seneta wa Nandi, Samson Cherargei
Image: Facebook//Cherargei

Seneta wa Nandi Samson Cherargei amesema kuwa wanachama wa muungano wa Azimio la Umoja wanapaswa kuondolewa serikalini kwa sababu hawaungi mkono uongozi wa Rais William Ruto.

Seneta Cherargei anaamini kuwa “mabaki” wote wa Azimio katika utumishi wa umma wanafaa “kusafishwa” ili kuzuia mipango ya Rais Ruto kuhatarishwa.

Cherargei alisema Jumatano kwamba pendekezo lake tayari limetekelezwa katika uteuzi wa Makatibu wa Baraza la Mawaziri (CSs) na Makatibu Wakuu (PSs), na kwamba ngazi zingine za serikali hazipaswi kuachwa.

"Katika serikali hii, bado kuna mabaki mengi wa Azimio One Kenya Alliance katika nyadhifa za juu na wanapaswa kuonyeshwa mlango. Hakuna chaguo," alisema akizungumza kwenye Spice FM.

Seneta huyo wa Nandi aliendelea kudai kuwa hakuna maana kuwa na watumishi wa umma wanaofanya kazi chini ya rais wanayempinga na badala yake wabadilishwe na wale wanaounga mkono “maono” ya Rais.

"Hawa ni watu ambao walijulikana kutomheshimu rais alipokuwa naibu, walimpigia kampeni mgombea mwingine lakini unawezaje kuhudumu chini yangu wakati hukumheshimu. amini katika maono yangu," Cherargei alisema.

“Ndio maana utaona hujuma za hapa na pale na kwa maoni yangu kusema kweli pata watu wanaoamini katika maono yako, wasafishwe mabaki wa Azimio waliomo ndani ya mfumo."