Uchumi mbaya: Kampuni ya usafiri wa ndege ya 748 Air yasitisha huduma zake Kenya

Kampuni hiyo ilianza kutoa huduma za usafiri wa ndani nchini mnamo Mei mwaka 2021.

Muhtasari

• Kampuni hiyo inatoa huduma za kibinadamu kwa mataifa 7 Afrika ambapo lengo lao ni kueneza amani na kupiga vita njaa.

Kampuni ya 748 Air yaondoka Kenya.
Kampuni ya 748 Air yaondoka Kenya.
Image: Facebook

Kampuni ya usafiri wa angani nchini Kenya 748 Air imetangaza kusitisha huduma zake za ndani katika anga la Kenya.

Kupitia kwa barua ambayo kampuni hiyo ya ndege ilipakia kwenye mtandao wao wa Facebook, walisema kwamba uamuzi wao wa kusitisha safari zao za ndani Kenya uliafikiwa baada ya tathmini ya muda mrefu kiuchumi.

“Baada ya tathmini ya kina kuhusu mbinu zetu za kibiashara, tumeafikia kujikita Zaidi katika lengo letu kuu la kutoa msaada wa kibinadamu wa usafiri wa ndege ambao tayari unaendelea katika mataifa 7 Afrika. Kwa hivyo, tunajuta kuwataarifu kwamba tumeamua kusitisha huduma zetu katika anga la ndani zilizokuwa zimeratibiwa. Huduma zote zinasitishwa kuanzia Machi mosi,” sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.

748 Air walianza kutoa huduma zao za usafiri katika anga la Kenya mnamo Mei mwaka 2021 na wametangaza kuanzisha mchakato wa kuwarudishia nauli wasafiri wote wa ndani ambao walikuwa wameratibu safari zao.

“Mfumo wetu wa ARS utasalia wazi mpaka mwisho wa mwezi Juni mwaka huu ili kuwezesha kurudisha nauli kwa tikiti zote ambazo zilikuwa zimenunuliwa. Lengo letu ni kuunganisha ubinadamu kupitia kwa kila safari ya angani kwa kushirikiana na wadau wengine katika kukuza na kueneza Amani na kupiga vita njaa Afrika,” taarifa hiyo ilisema.

Mfumuko wa uchumi katika mataifa mengi duniani umekuwa ukiathiri biashara na makampuni mbalimbali tangu ujio wa janga la Covid-19.

Mwaka jana, kampuni ya usafiri wa teksi, NoPea Ride walitangaza kusitisha huduma zao nchini wakifuatiwa na kufungwa kwa mgahawa wa Hilton ambao ulikuwa umeteka jiji la Nairobi kwa Zaidi ya miongo 3.