Thika: Washukiwa 3 wa ukabaji wachomwa moto baada ya kumpokonya mwanamke pochi

Visu vitatu vya washukiwa, simu ya rununu na vifaa vya kibinafsi vilivyoibiwa kutoka kwa mwathiriwa vilipatikana.

Muhtasari

• Watatu hao walimpokonya mwanadada pochi lake wakiwa kwa pikipiki kabla ya kuanza kutoroka.

Wanaume watatu wanaoshukiwa kuwa wakabaji walipoteza maisha yao baada ya umati wenye ghadhabu kuwavamia na kuwakandamiza hadi kupoteza maisha, baada ya kumpokonya mkoba mwanamke katika eneo la Thika Makongeni, Kaunti ya Kiambu.

Kulingana na DCI, Watatu hao waliokuwa kwenye pikipiki walikuwa wamemvamia mwanamke mmoja aliyekuwa akifanya biashara yake katika eneo la Polysack kabla ya kutoroka kuelekea mjini Thika kwa pikipiki nyekundu ambayo namba zake za usajili hazikuwepo.

Mayowe ya mwanamke huyo ya dhiki yaliwapata waendesha bodaboda na vijana wengine wachache waliokuwa wametulia kwenye kibanda cha pikipiki jirani wakisubiri wateja, kwa mshangao.

Hili liliwafanya waendesha bodaboda kukimbiza pikipiki hiyo kwa mwendo wa kasi, kwani si chini ya pikipiki 30 zilipita kwenye barabara kuu yenye shughuli nyingi zikitafuta damu ya watatu hao walioelekea Thika kujikomboa.

Wezi hao walipokuwa wakitoroka, ghafla matatu ilitokea na vijana hao walipokuwa wakijaribu kukwepa gari hilo walipigana dafrau na ukuta wa barabara na kupukutika sakafuni.

“Kilichofuata hapo ni kipigo ambacho majambazi hao hawakuwahi kukipata maishani mwao huku waendesha bodaboda wakiwashukia kwa makofi na mateke wakiwatuhumu kuwachafua kwa kutumia pikipiki kama chombo cha uharifu baada ya kufanya uhalifu,” DCI waliripoti.

Hadi maafisa wa polisi waliokuwa wakihudumia dharura nyingine wanafika, watatu hao kwa bahati mbaya walikuwa wamepondwa mithili ya majani na miili yao kuchomwa moto.

Polisi walihamisha mabaki yao yaliyokuwa yameteketea hadi katika chumba cha maiti cha hospitali ya General Kago ili kusubiri kutambuliwa na jamaa zao.

Wakati huo huo, visu vitatu vya washukiwa, simu ya rununu na vifaa vya kibinafsi vilivyoibiwa kutoka kwa mwathiriwa vilipatikana.