DCI waomba msamaha baada ya kuchapisha picha bandia za maandamano ya Azimio

Baadhi ya picha hata hazikupigwa nchini Kenya.

Muhtasari

•Picha nyingi walizoonyesha wakidai ni za maandamano ya Jumatatu hazikuchukuliwa wakati wa maandamano ya hivi majuzi.

•DCI wamesema mkanganyiko huo mkubwa ulisababishwa na taarifa nyingi walizopokea kutoka kwa wananchi.

na baadhi ya picha ghushi zilizochapishwa na DCI.
Mkurugenzi wa DCI Mohammed Amin na baadhi ya picha ghushi zilizochapishwa na DCI.
Image: HISANI

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini Kenya (DCI)  imeomba msamaha kwa umma baada ya kuchapisha picha za kutatanisha siku ya Ijumaa.

Siku ya Ijumaa, maafisa wa DCI walitangaza kwamba wameanzisha msako dhidi ya washukiwa walionaswa kwenye kamera wakijihusisha na vitendo vya vurugu wakati wa maandamano ya Azimio siku ya Jumatatu.

Hata hivyo, baadaye ilibainika kuwa picha nyingi walizoonyesha kwenye kurasa zao rasmi za mitandao ya kijamii wakidai ni za maandamano ya Jumatatu hazikuchukuliwa wakati wa maandamano ya hivi majuzi.

Katika utetezi wake, DCI wamesema mkanganyiko huo mkubwa ulisababishwa na taarifa nyingi walizopokea kutoka kwa wananchi.

Wakati tunajitahidi kurekebisha hali hiyo na kudumisha imani ya umma katika shughuli zetu, Kurugenzi inaendelea kutoa wito kwa umma kwa taarifa kuhusu waliko washukiwa ambao picha zao zinaonekana hapa chini.

"Wakati tunajitahidi kurekebisha hali hiyo na kudumisha imani ya umma katika shughuli zetu, Kurugenzi inaendelea kutoa wito kwa umma kutoa taarifa kuhusu waliko washukiwa ambao picha zao zinaonekana hapa chini," wapelelezi waliandika na kuambatanisha ujumbe huo na picha  walizodai ni za washukiwa.

Siku ya Ijumaa, idara ya DCI ilisema kuwa wameanzisha uchunguzi kuhusu matukio ya ghasia ambayo yalishuhudiwa wakati wa maandamano ya  siku ya Jumatatu ambayo waliyataja kuwa haramu.

Waliendelea kusambaza picha ambazo walidai zilipigwa wakati wa maandamano hayo kabla ya Wakenya kugundua zingine zilikuwa za zamani hadi zaidi ya mwongo mmoja uliopita. Baadhi ya picha hata hazikupigwa nchini Kenya.

"Kwa sasa Kurugenzi inaendelea na msako wa kuwatafuta washukiwa ambao picha zao zinaonekana huku za wengine zikikusanywa na zitachapishwa, ambao watakabiliwa na mashtaka kuanzia wizi wa kimabavu, uharibifu wa mali ya umma na shambulio kati ya makosa mengine yanayohusiana. Tunatoa wito kwa umma kujitolea habari ambazo zinaweza kusababisha kukamatwa kwao," walitangaza.

Moja ya picha inayoonyesha waandamanaji wakiruka kizuizi kilichokuwa kinawaka wakati wakiandamana ilichapishwa na CNN mnamo Mei 1, 2015 na ilikuwa ni waandamanaji nchini Burundi baada ya rais wa wakati huo Pierre Nkurunziza kuteuliwa na chama chake cha kisiasa CNDD-FDD kugombea uchaguzi wa urais wa 2015.

Picha nyingine ya muandamanaji akirusha jiwe ilichapishwa kwa mara ya kwanza na Financial Times mnamo Januari 10, 2018.