Gavana Sakaja aanzisha uboreshwaji wa mochwari ya City, "Maiti inahitaji heshima"

Sakaja alisema tayari makabati ya kuongeza baridi kwa maiti yamewekwa mapya kwenye vyumba vya kuhifadhi maiti.

Muhtasari

• “Kuhifadhi utu wa marehemu wetu na familia zao kwa kuboresha Hifadhi ya Maiti ya Jiji pamoja na makaburi yetu,” gavana Sakaja alisema.

Gavana Sakaja aanzisha kuboreshwa kwa mochwari ya City.
Gavana Sakaja aanzisha kuboreshwa kwa mochwari ya City.
Image: Twitter

Kwa muda mrefu kumekuwa na lalama kutoka kwa baadhi ya watu kuhusu hali duni ya makafani ya kaunti ya Nairobi ya City.

Makafani ya City yanajulikana kama sehemu ambayo maiti ambazo hazijatambulika hurundikwa zikisubiria wenyewe kuzitambua.

Aghalabu, miili mingi ambayo hurundikwa kwenye makafani hiyo ni ile ya watu waliouawa na kutupwa sehemu mbalimbali jijini Nairobi na maeneo yanayozunguka jiji, wale amabo hujitoa uhai na wale wanaofariki katika ajali za barabarani.

Polisi huchukua miili hiyo na kuirundika katika makafani ya City, ikisubiriwa wenyewe kuitambua, na hili hufanya makafani hiyo kufurika miili isiyo na wenyewe muda mwingi.

Gavana Sakaja sasa amechukua hatua ya kuboresha huduma katika makafani hiyo ya serikali, akisema kwamba maiti nao inahitaji heshima pamoja na wapendwa wao wanaoenda kuchukua miili ile kwa ajili ya heshima za mwisho.

“kuhifadhi utu wa marehemu wetu na familia zao kwa kuboresha Hifadhi ya Maiti ya Jiji pamoja na makaburi yetu,” gavana Sakaja alidokeza kupitia Twitter.

Gavana huyo alidokeza pia kwamba tayari makabati ya kuhifadhi miili mapya yameshawekwa pamoja na huduma zingine ambazo zilikuwa duni hapo awali.

“Ufungaji wa makabati mapya ya baridi, milango ya chumba cha baridi na kazi za mifereji ya maji (kamili). Mkandarasi yuko kazini. Hatua kwa hatua. Lazima kila kitu iWork,” Sakaja alisema akionesha sehemu ya makafani hiyo katika sura mpya.